2013-05-07 07:33:37

Mshikamano wa Vatican na Kanisa la Tanzania kutokana na vitendo vya kigaidi vinavyopelekea mauaji ya watu wasiokuwa na hatia!


Askofu mkuu Francisco Padilla, Balozi wa Vatican nchini Tanzania aliyenusurika kwa kifo Jumapili iliyopita wakati bomu liliporushwa kwenye Kanisa la Parokia ya Mtakatifu Yosefu Mfanyakazi Olasiti, Jimbo kuu la Arusha, anasema kwamba, kama Mwakilishi wa Baba Mtakatifu Francisko anapenda kuonesha moyo wa mshikamano na upendo wa dhati kwa waamini wa Jimbo kuu la Arusha na Kanisa la Tanzania kwa ujumla kutokana na kitendo hiki ambacho kimewaacha wengi wakiwa wameshikwa na mshtuko mkubwa. RealAudioMP3

Anawaombea wale waliofariki dunia ili waweze kupata pumziko la amani na majeruhi waweze kupona haraka na kuendelea na shughuli zao bila ya kukata tamaa!

Askofu mkuu Francisco Padilla ameyasema haya wakati wa mahojiano maalum na Radio Vatican kwa kukazia kwamba, kwa mara ya kwanza mlipuko wa bomu umtokea kwenye Kanisa Katoliki, tofauti na nchi nyingine kama vile Kenya ambako matukio kama haya yamejirudia mara kadhaa wakati wa Liturujia. Ameonesha masikitiko makubwa kwa vitendo vya uchomaji wa Makanisa na madhulumu kwa viongozi wa kidini yanayojitokeza nchini Tanzania. Ni matumaini yake kwamba, hali ya amani na usalama itarejea tena nchini Tanzania.

Askofu mkuu Padilla anasema kwamba, walipokuwa wanakaribia kuanza ibada ya misa Takatifu akisaidiana na Askofu mkuu Josephat Lebulu wa Jimbo kuu la Arusha, alisikia mlipuko wa bomu na mara baada ya kitambo kidogo akaona watu kadhaa wakiwa wamejeruhiwa. Vyombo vya ulinzi na usalama vimamchukua na kumpatia hifadhi wakati ambapo juhudi za kuokoa maisha ya wale walioumia zikiwa zinaendelea.

Askofu mkuu Padilla anasikitika zaidi kwa watu walioumia kwa kuwa walikuwepo kwenye Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kutabaruku Kanisa, kama sehemu ya Maadhimisho ya Jubilee ya Miaka 50 ya Jimbo Kuu la Arusha sanjari na Maadhimisho ya Mwaka wa Imani. Inasikitisha kuona watu wasiokuwa na hatia wanapoteza maisha na kupata hata vilema vya kudumu kutokana na imani yao kwa Kristo na Kanisa lake!

Balozi wa Vatican anasema, Serikali ya Tanzania imemhakikishia kwamba, itafanya uchunguzi wa kina ili kuwakamata wahusika na kuwafikisha kwenye mkondo wa sheria. Rais Jakaya Kikwete wa Tanzania pamoja na viongozi wakuu wa Tanzania wameshutumu sana kitendo hiki na kukiita kuwa ni kitendo cha kigaidi kinachotaka kuvuruga amani na mshikamano wa kitaifa.

Wakati huo huo, Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania amewataka wakristo kuwa na subira na kamwe wasikate tamaa kwani Mwenyezi Mungu atatoa majibu kwa wakati muafaka. Amewataka watanzania kuendeleza upendo na haki kwani hizi ni zawadi kutoka kwa Mungu. Watu waendelee kufunga na kusali kwa ajili ya kuombea: haki, amani, upendo na mshikamano wa kitaifa. Wale waliopoteza maisha yao wapate rehema kwa Mungu wapumzike kwa amani na majeruhi wafarijike kwa sala na sadala zinazotolewa na waamini wakati huu.







All the contents on this site are copyrighted ©.