2013-05-07 09:50:37

Bikira Maria anawasaidia waamini kukua, kukabiliana na changamoto za maisha na hatimaye, kuwa huru!


Baba Mtakatifu Francisko wakati wa kusali Rozari takatifu kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria Mkuu lililoko Mjini Roma, Jumamosi iliyopita, alikazia kwa namna ya pekee nafasi na dhamana ya Bikira Maria katika maisha ya wafuasi wa Kristo. Bikira Maria anawasaidia waamini kukua, kukabiliana na changamoto za maisha na hatimaye kuwa huru!

Kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko; Yesu Kristo anamkirimia mwanadamu maisha ya uzima wa milele na kumpatia neema ya kuwa kweli ni mwana mteule wa Mungu, kiasi hata cha kudiriki kumwita, Baba! Bikira Maria kwa upande wake ni Mama anayejali afya ya watoto wake; akiwasaidia kukua na kukomaa ili kuweza kukabiliana na changamoto za maisha, wakiwa huru kutenda kadiri ya Mpango wa Mungu.

Mama mwema anasema Baba Mtakatifu Francisko anawafundisha watoto wake kukua salama, huku wakiwa ni wachapa kazi, ili kuwajibika katika maisha yao kwa sasa na kwa siku za usoni; wakiwa na ndoto na matarajio ya maisha. Bikira Maria anawasaidia waamini kukua na kukomaa katika utu na maisha ya imani; wakiwa thabiti katika kukabiliana na vishawishi vya maisha. Anawataka wakristo kuwa imara katika imani daima wakiwajibika vyema katika Jamii na Kanisa kwa ujumla.

Mama mwema anawafundisha watoto kukabiliana na changamoto pamoja na ugumu wa maisha, kwani kama binadamu, watakumbana na vikwazo katika safari yao hapa duniani. Kumbe, watoto hawana budi kufundishwa kuwa na moyo wa ujasiri na ukakamavu, pamoja na mbinu za kuweza kukabiliana na hali mbali mbali za maisha bila kuogopa wala kukata tamaa! Hakuna maisha ya raha mustarehe kabisa anasema Baba Mtakatifu Francisko. Watoto wafundishwe mahali ambapo wanaweza kuwa na usalama na sehemu ambazo maisha yao yanaweza kuwa hatarini.

Bikira Maria ni mwanamke wa shoka! Aliyeonja shida na magumu katika maisha yake, tangu kuzaliwa kwa Yesu Kristo hadi pale aliposimama chini ya Msalaba akamwona Mwanaye wa Pekee, akiinamisha kichwa na kukata roho! Uchungu wa Mwana anasema Baba Mtakatifu anaujua mzazi! Pale chini ya Msalaba, wafuasi wote wa Kristo walikabidhiwa chini ya usimamizi na ulinzi wa Bikira Maria anayewaonesha njia inayokwenda kwa Yesu.

Mama mwema anamsaidia mtoto wake kuwa huru, akiwa na vigezo sahihi vya kufanya maamuzi makini katika maisha; akitambua mema yakufuata na mabaya yakuepuka! Bikira Maria anawasaidia waamini kufanya maamuzi makini ya maisha, huku wakiwa huru kabisa kama alivyofanya yeye mwenyewe alipokubali Mpango wa Mungu katika maisha yake. Ulimwengu mamboleo umesheheni vishawishi ambavyo waamini wanapaswa kuviepuka kwa kuonesha ujasiri.

Bikira Maria afya ya watu wa Roma ni kimbilio la wengi, kwa wale wanaomwomba: imani, matumaini na mapendo katika maisha yao. Ni mwanamke anayewahimiza wafuasi wa Kristo kujikita katika matendo ya huruma, kwa kujitoa kuwasaidia wengine ambao wanashida na mahangaiko mbali mbali ya maisha.

Kila mtu anaalikwa kuwa ni chombo bora cha maisha. Baba Mtakatifu Francisko anawakumbusha waamini kwamba, Bikira Maria ni Mama wa Yesu na Kanisa. Anawaomba kuendelea kumkumbuka katika maisha na utume wake! Hii ndiyo changamoto inayowakabili wanawake katika Mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo, kila mtu atekeleze wajibu wake, yote haya yanawezekana!







All the contents on this site are copyrighted ©.