2013-05-06 14:23:30

Watu sita watiwa pingu kuhusiana na shambulizi la Kigaidi, Jimbo kuu la Arusha!


Kanisa Katoliki nchini Tanzania linasubiri kupata habari za uhakika kutokana na shambulio la kigaidi lililotokea Jimbo kuu la Arusha, wakati Askofu mkuu Francisco Padilla, Balozi wa Vatican nchini Tanzania akiwa pamoja na Askofu mkuu Josephat Lebulu tayari kuanza Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kutabaruku Kanisa la Parokia ya Mtakatifu Yosefu Mfanyakazi Olasiti, Jimbo kuu la Arusha, Jumapili tarehe 5 Mei 2013 kabla ya kutoa tamko lake.

Askofu mkuu Padilla ambaye amekuwemo Jimboni humo tangu tarehe 2 Mei 2013 ameendelea na ziara yake ya kichungaji kwa kuzungumza na Makleri wa Jimbo kuu la Arusha. Kwa kipindi cha miezi ya hivi karibuni, Wakristo nchini Tanzania wamekuwa ni walengwa wa mashambulizi ya kidini ingawa kuna kundi kubwa la Waamini na Viongozi wa dini ya Kiislam ambao wameendelea kuunga mkono jitihada za kujenga na kudumisha upendo, umoja na mshikamano wa kitaifa.

Shirika la Habari za Kimissionari linabainisha kwamba, hadi sasa kuna watu 6 wametiwa pingu na kati yao kuna watu 4 ni wananchi kutoka Saud Arabia, ambao wanahusisha na shambulizi hili la kigaidi, ambalo limeshutumiwa na viongozi mbali mbali wa Tanzania na wapenda amani kwa ujumla. Habari hizi zimethibitishwa pia na Mkuu wa Mkoa wa Arusha Bwana Magesa Mulongo na kuongeza kwamba, dereva wa Piki piki iliyotumika katika shambulio hili la kigaidi ni kati ya wale waliotiwa mbaroni.







All the contents on this site are copyrighted ©.