Mchango wa Kanisa katika kupambana na baa la umaskini duniani!
Kardinali Oscar Rodriguez Maradiaga, Rais wa Shirikisho la Mashirika ya Misaada ya
Kanisa Katoliki Kimataifa, Caritas Internationalis, tarehe 10 Mei 2013 atatunukiwa
Shahada ya Udaktari wa heshima kutoka Chuo Kikuu cha Parma, kilichoko nchini Italia,
kutokana na mchango wake mkubwa katika mapambano dhidi ya baa la umaskini duniani.
Kardinali Maradiaga atatoa mhadhara kuhusu maadili na maendeleo endelevu.
Kardinali
Maradiaga amekuwa mstari wa mbele kusimama kidete kulinda na kutetea haki msingi za
binadamu na maendeleo endelevu kwa wananchi wa Amerika ya Kusini pamoja na sehemu
mbali mbali za dunia. Mapambano haya wakati mwingine yamehatarisha hata maisha yake
kutokana na baadhi ya “vigogo” kumwona kwamba, anaweka kizingiti katika mikakati yao
ya kujipatia utajiri mkubwa kwa kuwanyonya na kuwadhulumu maskini na watu wasiokuwa
na sauti.
Ni kiongozi ambaye amejitahidi kadiri ya uwezo wake kumwilisha mafundisho
Jamii ya Kanisa kama dira na mwelekeo wa vipaumbele vyake katika utekelezaji wa mikakati
ya shughuli za kichungaji. Kardinali Oscar Maradiaga kwa hakika ni Baba, Mwalimu na
Kiongozi, ambaye Wanazuoni wameutambua mchango wake na kwa sasa anatunukiwa Shahada
ya Udaktari wa heshima kutoka Chuo Kikuu cha Parma kilichoko nchini Italia.