2013-05-06 10:58:08

Malaria bado ni tishio Barani Afrika


Jumuiya ya Kimataifa haina budi kuendeleza mapambano yake dhidi ya ugonjwa wa Malaria ambao bado ni chanzo kikuu cha vifo vya watoto wengi Barani Afrika. Takwimu za Umoja wa Mataifa zinaonesha kwamba, katika kipindi cha Mwaka 2010 kulikuwa na wagonjwa wa Malaria million 219 na kati yao wagonjwa 655,000 walipoteza maisha yao.

Taarifa ya Shirika la Afya Duniani iliyotolewa hivi karibuni inaonesha kwamba, asilimia 90% ya vifo vyote ni kutoka Barani Afrika na kwamba, Afrika ina idadi kubwa zaidi ya wagonjwa wa Malaria.

Kumekuwepo na maendeleo makubwa katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa Malaria Kimataifa kwa kupunguza vifo vya ugonjwa huu kwa asilimia 25% katika kipindi cha miaka kumi iliyopita. Lakini bado kuna idadi kubwa ya wagonjwa wa Malaria wanaendelea kupoteza maisha Barani Afrika, wengi wao ni watoto wenye umri chini ya miaka mitano. Malaria ni ugonjwa ambao unaweza kudhibitiwa ikiwa kama watunga sera na wananchi wataonesha utashi wa kupambana kufa na kupona na ugonjwa wa Malaria.

Ikiwa kama watu watatumia vyema vyandarua vilivyowekwa dawa, wakatunza usafi wa mazingira na kutumia dawa sahihi, kuna uwezekano mkubwa wa kupunguza vifo vya watoto wadogo vinavyotokana na ugonjwa wa Malaria Barani Afrika. Takwimu zinaonesha kwamba, kati ya watoto 10 nchini Cameroon, 3 wana hatari kubwa ya kupata ugonjwa wa Malaria ambao ni kati ya changamoto kubwa za mikakati ya afya nchini Cameroon.







All the contents on this site are copyrighted ©.