Askofu Mkuu Francisco Padilla, Balozi wa Vatican nchini Tanzania, Askofu mkuu Josephat
Lebulu wa Jimbo kuu la Arusha, Mapadre, Watawa pamoja na waamini waliokuwa wamekusanyika
kwenye Maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kutabaruku Kanisa la Parokia
ya Mtakatifu Yosefu Mfanyakazi Olasiti, Jimbo kuu la Arusha, wamenusurika kwa kifo
baada ya bomu kurushwa kwenye eneo la Kanisa na kulipuka, Jumapili tarehe 5 Mei 2013.
Taarifa
zinabainisha kwamba, watu watatu tayari wamekwisha fariki dunia na kuna majeruhi 66
wanaoendelea kupata matibabu Jijini Arusha. Baada ya shambulizi hili, Ibada ya Misa
Takatifu haikuweza kuendelea na hapo harakati za kuokoa maisha ya waamini zikaanza
mara moja.
Ibada ya Misa takatifu ilikuwa inaongozwa na Askofu mkuu Francisko
Padilla, ambaye amekuwepo Jimboni Arusha tangu tarehe 2 Mei 2013 kwa ajili ya ziara
ya kikazi kama sehemu ya Maadhimisho ya Jubilee ya Miaka 50 ya Jimbo kuu la Arusha.
Wachunguzi wa masuala ya kidini wanasema, hii ni changamoto kwa Wakristo nchini
Tanzania wakati huu wa Maadhimisho ya Mwaka wa Imani sanjari na Jubilee ya Miaka 50
ya Jimbo kuu la Arusha wanapoendelea kuhimizwa na viongozi wa Kanisa kutolipiza kisasi,
lakini Serikali na Vyombo vya ulinzi na usalama vinapaswa kutekeleza wajibu wake ili
wahusika waweze kufikishwa kwenye mkondo wa sheria kwani matukio kama haya yanaendelea
kujenga hofu, chuki na uhasama kati ya watanzania, jambo ambalo ni hatari kabisa kwa
maendeleo na ustawi wa watanzania.