Ukweli kuhusu marekebisho ya kina ndani ya Kanisa!
Baba Mtakatifu Francsiko hivi karibuni aliteuwa kikundi cha Makardinali wanane kutoka
sehemu mbali mbali za dunia, kitakachomsaidia kupata mawazo ya kufanya marekebisho
ya uongozi wa Kanisa la Kiulimwengu pamoja na kuangalia uwezekano wa kufanya mabadiliko
kwenye Waraka wa kichungaji, “Pastor Bonus” mchungaji mwema.
Hii ni sehemu
ya utekelezaji wa mawazo yaliyotolewa na Makardinali wakati wa mikutano yao elekezi
kabla ya uchaguzi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro. Uamuzi wa Baba Mtakatifu Francisko
umezua hisia ambazo nyingine zimekwenda hata kinyume cha mawazo ya Baba Mtakatifu
Mwenyewe, kila mtu akitaka kuweka walau chumvi kwa kile anacho amaini hasa kuhusiana
masuala ya uongozi, mikakati na sera za uchumi wa Vatican na mageuzi katika ujumla
wake.
Askofu mkuu Angelo Becciu, Katibu Mwambata wa Vatican katika mahojiano
maalum na Gazeti la L’Osservatore Romano linalotolewa na kila siku mjini Vatican anabainisha
kwamba, kuna baadhi ya waandishi wa habari wametia chumvi mno, kwani hadi sasa Baba
Mtakatifu Francisko hajaonesha wazi utashi wake juu ya muundo wa Ofisi za wasaidizi
wake wa karibu walioko mjini Vatican.
Kwa sasa Baba Mtakatifu anaendelea kusikiliza
ushauri kutoka kwa watu mbali mbali, lakini atapenda kusikiliza zaidi ushauri makini
utakaotolewa na Kundi la Makardinali wanane aliowachagua kwa ajili ya kazi hii nyeti
ndani ya Kanisa. Kwa vile kuna haja ya kufanya mabadiliko katika Waraka wa Mchungaji
mwema, kumbe, kunahitajika kwanza kabisa mwongozo makini utakaoelekeza mchakato mzima,
ili yote yafanyike kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Kanisa la Kristo.
Askofu
Becciu anasema, kuna baadhi ya watu wamekwenda mbali kiasi cha kusema kwamba, Baba
Mtakatifu Francisko anatarajia kufunga Benki ya Vatican kwa vile haina umuhimu wowote,
jambo ambalo si kweli kabisa. Kuna siku wakati wa Maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu
iliyowashirikisha wafanyakazi kutoka Benki ya Vatican, alizungumzia kuhusu kiini cha
maisha na utume wa Kanisa kwamba, kinajionesha kwa namna ya pekee katika uhusiano
wa upendo kati ya Mungu na binadamu. Kumbe hata taasisi kubwa kama Benki ya Vatican
haina budi kutoa mwelekeo huu ambao n ikiini na utambulisho wa Kanisa, vinginevyo
haina maana ya kuwapo!
Mabadiliko yanayokusudiwa na Baba Mtakatifu Francisko
yatakuja kwa wakati wake, lakini kwa sasa Wasaidizi wake wa karibu wanaendelea kutekeleza
majukumu yao kama alivyowataka yeye mwenyewe. Wakuu wa “Curia” wanayo dhamana ya kuongoza
Mabaraza ya Kipapa kwa kipindi cha miaka mitano, inapomalizika miaka hii, Baba Mtakatifu
anakuwa na uamuzi wa kuuisha mkataba au kufanya uteuzi wa kiongozi mwingine. Baba
Mtakatifu amesema kwamba, anahitaji muda wa kufanya tafakari ya kina pamoja na kusali
ili kupata hali halisi ya uongozi wa Vatican kabla ya kufanya maamuzi yake.
Askofu
mkuu Angelo Becciu anasema, Papa ndiye kiongozi mkuu wa Kanisa Katoliki na mwenye
uamuzi wa mwisho. Makardinali walioteuliwa kumshauri hawa wanabaki kuwa ni washauri,
hiki ni kielelezo makini kinachoonesha jinsi ambavyo Baba Mtakatifu Francisko anavyotaka
kutekeleza wajibu wake wa kuongoza, kufundisha na kuwatakatifuza watu wa Mungu.
Makardinali
hawa wamepewa dhamana ya kumashauri Baba Mtakatifu katika utekelezaji wa utume wake
kwa Kanisa la kiulimwengu. Mabadiliko ya muundo wa Curia usiwe ni “kiwingu” cha kutaka
kupotosha utashi na dhamiri nyofu ambayo imeoneshwa na Baba Mtakatifu Francisko katika
kuleta mabadiliko ndani ya Kanisa, kama walivyoshauri pia Makardinali wakati wa mikutano
yao elekezi kabla ya uchaguzi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro.
Ushauri unapaswa
kufahamika mintarafu taalimungu kama inavyofafanuliwa na Mama Kanisa. Askofu mkuu
Angelo Becciu anasema, hata katika ngazi ya Parokia na Majimbo, Kanisa limeweka utaratibu
wa kuwa na washauri , ambao baada ya kutoa ushauri wao, maamuzi yanafanywa na Mhusika
mkuu, kama ni Jimbo, basi yanafanywa na Askofu, kama ni katika ngazi ya Parokia, basi
Paroko husika anatekeleza utume wake kadiri ya Sheria na Kanuni za Kanisa.
Ushauri
huu ni huduma ili kusoma alama za nyakati, ili kutambua Roho Mtakatifu anataka nini
kutoka kwa Kanisa wakati huu wa Mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo. Uongozi
ndani ya Kanisa ni huduma!