2013-05-04 08:20:19

Nia za jumla na kimissionari za Papa kwa Mwezi Mei, 2013


Baba Mtakatifu Francisko katika nia zake za jumla kwa Mwezi Mei 2013 anasali ili kwamba, viongozi waliopewa dhamana ya kutoa haki, wahakikishe kuwa wanatenda kwa unyofu huku wakiongozwa na dhamiri nyofu.

Anakumbusha kwamba, amani ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu, inayowawajibisha watu ndani ya Jamii, ili kujenga uhusiano unaojikita katika msingi wa haki na mshikamano wa dhati, sanjari na kuheshimu kazi ya uumbaji ambayo binadamu amepewa dhamana ya kuitunza na kuiendeleza kwani hii, ni sehemu ya mchakato wa kazi ya ukombozi na maana ya uwepo wa mwanadamu hapa duniani.

Huu ni mchakato unaoongozwa na sheria na kanuni zilizoandikwa katika dhamiri ya mwanadamu, hali inayoonesha mpango wa Mungu. Amani kama alivyowahi kusema Mwenyeheri Yohane Paulo wa pili ni mwaliko wa kuishi na kutenda kadiri ya Mpango wa Mungu na kwamba, dhamiri nyofu na uhuru kamili ni njia ya kutekeleza Mpango wa Mungu kwa binadamu wote. Haya ni mambo yanayopaswa kupokelewa kwa moyo wa dhati na wala si kama shinikizo kutoka nje ya maisha ya binadamu. Kwa mwelekeo kama huu, binadamu kutoka katika tamaduni mbali mbali anaweza kumkaribia Mwenyezi Mungu.

Kuna haja ya kuheshimu sheria asilia ambayo imeandikiwa katika dhamiri ya mwanadamu kama msingi wa majadiliano ya kidini na kiekumene ili kujenga na kudumisha haki na amani duniani. Ukosefu wa haki na usawa ni chanzo kikuu cha kinzani na migogoro ya kivita sehemu mbali mbali za dunia. Umaskini, baa la njaa, ukosefu wa huduma ya maji safi na salama; ukosefu wa makazi bora, huduma za afya na elimu; yameendelea kuwa ni chanzo kingine cha migogoro ya kijamii Barani Afrika. Kumbe, haya ni mambo msingi yanayopaswa kuzingatiwa ili Jamii iweze kuwa na amani na utulivu.

Baba Mtakatifu anawachangamotisha kwa namna ya pekee viongozi waliopewa dhamana ya kutoa haki katika ngazi mbali mbali za maisha ya kijamii, kutambua kwamba, pasi na haki, amani iko mashakani. Mahakimu wanapaswa kutekeleza wajibu wao kikamilifu wakiongozwa na ukweli pamoja na dhamiri nyofu. Kwa njia hii wataweza kuheshimiwa na kuthaminiwa ndani ya Jamii husika.

Kwa bahati mbaya, mambo ni kinyume kabisa na ukweli wa mambo; mahakimu wamekuwa wakishutumiwa kwa: rushwa, upendeleo na mashinikizo ya kisiasa kiasi kwamba, wanakosa heshima na Jamii nyingi zimekosa imani na Mahakimu wa namna ya hii.

Ikumbukwe kwamba, watu wana kiu ya haki, hii ni changamoto kwa Mahakimu katika ngazi mbali mbali kuhakikisha kwamba, wanatekeleza dhamana yao kwa moyo mnyofu, wakiongozwa na dhamiri nyofu inayomwezesha mwanadamu kuona jema linalopaswa kutendwa na baya kuepukwa!

Baba Mtakatifu Francisko katika nia yake ya Kimissionari kwa Mwezi Mei, 2013 anaziombea Seminari hasa zile ambazo zinapatikana kwenye nchi za Kimissionari ili zijitahidi kutoa majiundo makini kwa Makleri mintarafu Moyo wa Kristo, ili waweze kufundwa barabara, tayari kujitosa kimaso maso kwa ajili ya kutangaza Injili ya Kristo. Seminari ni Jumuiya inayoendeleza utume wa Kanisa la Mwanzo, wakristo walipokusanyika kusikiliza Injili ya Kristo pamoja na kuendeleza ile furaha na mang'amuzi ya Kipasaka, huku wakingojea ujio wa Roho Mtakatifu.

Utambulisho huu wa Seminari unakumbusha kwamba, Seminari pia ni Jumuiya ya Kibinadamu inayopaswa kuwa makini katika umwilishaji wa tunu msingi za maisha ya Kiinjili ili kusoma alama za nyakati na kujibu changamoto zinazoibuliwa katika ulimwengu wa sayansi na maendeleo ya teknolojia. Seminari inapaswa kujengeka katika msingi wa urafiki wa kweli na upendo ambao ni kielelezo makini cha Familia inayoishi katika furaha. Hii pia ni Jumuiya ya Kikanisa kama ambavyo Mababa wa Kanisa wanapenda kusema; kwani inaonesha ule uhusiano na Askofu au Mkuu wa Shirika husika.

Kutokana na mwelekeo huu, Seminari zinapaswa kuwa ni mahali ambapo majiundo ya Makleri kwa ajili ya maisha na utume wa Kanisa yanapata chimbuko lake, kama ilivyokuwa ile Seminari ya kwanza iliyoongozwa na Yesu Kristo mwenyewe, ikahudhuriwa na Mitume kumi na wawili kwa kipindi cha miaka mitatu! Hapa ni mahali pa majiundo ya kiakili yanayompatia mwombaji kujiandaa kikamilifu kabla ya kupewa Daraja Takatifu la Upadre, ili kutenda kama Kristo Kuhani mkuu na mchungaji mwema, aliyelidhaminisha Kanisa kuadhimisha Mafumbo ya Ukombozi.

Jumuiya ya Seminari kwa ujumla inashiriki katika majiundo ya Makleri; walezi wakitekeleza wajibu wao katika maisha ya: kiutu, kiroho, kiakili na kichungaji. Majandokasisi waelimishwe kutambua dhamana yao kama binadamu lakini zaidi kama viongozi wa kidini. Haya ni mambo yanayopaswa kukaziwa. Ni vyema, ikiwa kama Wakristo watajibidisha kwa mara nyingine tena, kujisomea ile Barua ya Kichungaji aliyoiandika Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita kwa Waseminari wakati wa Maadhimisho ya Mwaka wa Padre.







All the contents on this site are copyrighted ©.