2013-05-04 11:02:20

Majadiliano ya kidini ni njia ya kutolea ushuhuda wa imani!


Waamini wanachangamotishwa na Mama Kanisa kuwashirikisha waamini wa dini nyingine katika majadiliano ya kidini, kama njia ya kutolea ushuhuda wa imani yao kwa Kristo na Kanisa lake. Majadiliano ya kidini kati ya Wakristo na Waislam ni jambo ambalo linapaswa kupewa kipaumbele cha pekee kama sehemu ya mchakato wa Uinjilishaji mpya; fursa ya kuweza kufahamiana, kuheshimiana na kuthaminiana ili kujenga mshikamano wa upendo na kidugu utakaoimarisha misingi ya haki, amani na maendeleo ya kweli.

Viongozi wa dini hizi mbili wanapaswa kujibidisha zaidi katika majiundo ya waamini wao, ili waweze kufahamu kweli za imani za dini zao na utambulisho walio nao katika medani za kimataifa. Amani na utulivu vinaweza kudumisha ikiwa kama Jamii yenye imani na tamaduni tofauti itajifunza kuheshimu na kujitaabisha kufahamu kweli na imani za jirani zao kwa njia ya majadiliano endelevu.

Haya ni baadhi ya mawazo makuu yaliyojitokeza wakati wa mkutano wa tatu uliowajumuisha wajumbe kutoka Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Ulaya, uliokuwa unajadili uhusiano kati ya Waislam na Wakristo Barani Ulaya, uliofanyika mjini London, kuanzia tarehe Mosi hadi tarehe 3 Mei 2013.

Kardinali Jean Pierre Ricard, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Bordeaux alikazia kwa namna ya pekee umuhimu wa maajadiliano na utangazaji wa Habari Njema ya Wokovu kama njia ya majiundo yatakayowawezesha vijana wa Kiislam na Kikristo kupata utambulisho wao. Wajumbe wengine wamehimiza umuhimu wa ushuhuda kama njia ya kuzima changamoto zinazoendelea kujitokeza katika utekelezaji wa shughuli za kichungaji Barani Ulaya.

Wajumbe wanasema kuna haja kwa Kanisa Barani Ulaya kuendelea kuimarisha uwepo wake miongoni mwa vijana ilikuwasaidia katika majiundo na makuzi yao hatua kwa hatua. Majadiliano ya kidini na waamini wa dini ya Kiislam ni muhimu sana kwa kutambua kwamba, hata Waamini hawa wanatofautiana katika misimamo na kweli za imani zao kama ilivyo pia kwa Wakristo. Majadiliano yanayosimikwa katika: ukweli, uwazi na mafao ya wengi daima yatakuwa ni msaada mkubwa katika kudumisha misingi ya haki, amani na maendeleo endelevu kwa njia ya mshikamano wa kidugu.

Changamoto kubwa iliyoko mbele ya viongozi wa dini hizi mbili ni kuhakikisha kwamba, zinatoa majiundo makini kwa vijana kuhusu kweli za kiimani, kwa kukazia umuhimu wa elimu, maisha ya sala kama njia ya kukutana na kuzungumza na Mwenyezi Mungu; sala ambazo zinamwezesha mwamini kushirikiana na jirani zake. Elimu iwasaidie waamini kutambua tofauti zao za kiimani ambao ni utajiri mkubwa katika ujenzi wa Jamii inayowazunguka na wala si sababu ya kinzani na migogoro ya Kijamii. Waamini wajifunze kukataa misimamo mikali ya kiimani na badala yake wajenge utamaduni wa kusikilizana na kujadiliana.

Maendeleo ya sayansi na teknolojia katika ulimwengu wa utandawazi hasa Barani Ulaya, yawasaidie waamini wa dini hizi mbili kuangalia kuhusu umuhimu wa imani katika Jamii inayojipambanua katika uwezo wake wa kumiliki, kufanya na kutumia; mwelekeo ambao wakati mwingine unakwamisha uelewa sahihi wa uhusiano kati ya mwamini na Mwenyezi Mungu. Kutokana na hali kama hii, Kanisa halina budi kuendeleza mchakato wa majadiliano ya kidini na Waamini wa dini ya Kiislam. Mwamini wa dini yoyote ile atazamwe na kupimwa katika mizani ya familia na Jamii inayomzunguka kwani mwanadamu si kisiwa!

Majadiliano ya kidini wanasema wajumbe wa mkutano huu kwamba, ni hitaji la kimaadili na kitaalimungu ambalo ni endelevu. Pengine itachukua muda mrefu zaidi kuweza kufikia lengo lake, lakini waamini hawana haja wala sababu ya kukata wala kukatishwa tamaa.

Hii ni changamoto ya kuwekeza katika majadiliano ya kidini kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa Mwenyezi Mungu na binadamu, wakiongozwa na majitoleo na ukarimu hata pale ambapo jibu linaonekana kana kwamba, linachelewa kupatikana! Kwa hakika majadiliano ya kidini ni jambo ambalo linapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza nyakati hizi!







All the contents on this site are copyrighted ©.