2013-05-04 10:16:19

Maaskofu wa IMBISA kuanza kutumia mitandao ya kijamii kutuma ujumbe wa haki, amani na upendo!


Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Kusini mwa Afrika, IMBISA, hivi karibuni limehitimisha semina maalum iliyojikita katika matumizi sahihi ya mitandao ya kijamii inayoendelea kushika kasi kwa umaarufu, wepesi na kasi ya kuweza kuwafikia watu wengi kwa mkupuo, ikilinganishwa na njia za mawasiliano zilizozoeleka kama sehemu ya mapokeo.

Maaskofu katoliki kutoka Zimbabwe, baada ya kujifunza na hatimaye kuanza kubobea katika matumizi ya mitandao ya kijamii, wameamua kwamba, wakati wa mchakato wa uchaguzi mkuu nchini Zimbabwe watajitahidi kutumia kikamilifu mitandao hii ili kusambaza ujumbe wa amani, upendo, upatanisho na mshikamano wa kitaifa. Kwa njia ya mitandao, Maaskofu wataweza kuwafikia wananchi wa Zimbabwe wakiwa katika maisha yao ya kawaida, kuliko ilivyokuwa hapo hawali walipokuwa wanawasubiri wanapokwenda Kanisa siku za Jumapili.

Huu ni ufafanuzi kadiri ya taarifa za Shirika la Habari za Kanisa Barani Afrika, CISA, ambao umetolewa na Padre Richard Menatsi, Mkurugenzi wa Idara ya Mawasiliano IMBISA. Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Kusini Mwa Afrika, IMBISA linaonya kwamba, uchaguzi wa kidemokrasi haupaswi kamwe kuwa ni chanzo cha kinzani, vurugu na vita; lakini haya nimambo ambayo yamekuwa yakijitokeza sehemu mbali mbali Barani Afrika; daima waathirika ni raia na wanyonge ndani ya Jamii.

Umwefika wakati kwa wananchi Barani Afrika kujifunza kutumia kura zao kama njia makini inayoonesha utashi wa kisiasa unaopania kuleta mabadiliko. Ni wakati wa kujenga na kuimarisha misingi ya haki na amani na kwamba, matumizi ya mtutu wa bunduki ni mwelekeo ambao umepitwa na wakati!







All the contents on this site are copyrighted ©.