2013-05-04 07:32:39

Changamoto za kukuza na kudumisha misingi ya haki na amani katika Jumuiya ya Kimataifa!


Mama Kanisa anaendelea kuadhimisha Jubilee ya Miaka 50 tangu Baba Mtakatifu Yohane wa Ishirini na tatu, alipochapisha Waraka wa kichungaji “Pacem in Terris” Amani Duniani, zawadi kubwa kwa Jumuiya ya Kimataifa iliyokuwa inakabiliwa na changamoto nyingi kwa wakati ule. RealAudioMP3

Waraka huu ni ujumbe wa kinabii, lakini unaendelea kutoa changamoto kubwa kwa watu wa nyakati hizi. Kulikuwa na vitisho vya mashambulizi ya silaha za kinyuklia, jambo ambalo liliwakumbusha watu wengi madhara ya Vita kuu ya pili ya dunia.

Hiki ni kipindi ambacho Baba Mtakatifu Yohane wa Ishirini na tatu kwa ujasiri mkuu wa Kibaba na kichungaji, aliwaalika viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa na kila mtu kuhakikisha kwamba, anachuchumilia ujenzi wa misingi ya haki na amani pamoja na kusimama kidete kulinda na kutetea haki za binadamu; mwanadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu akipewa kipaumbele cha kwanza. Ni changamoto iliyokuwa inawagusa watu katika ngazi mbali mbali: kimataifa, kitaifa, kijamii na katika kukuza uhusiano kati ya mtu na mtu.

Waraka wa Amani Duniani unapata chimbuko lake katika Maandiko Matakatifu. Papa Yohane wa ishirini na tatu anachota ujumbe wake kutoka kwa mafundisho ya Manabii katika Agano la Kale na kuhitimisha na Ujumbe wa Amani ulioletwa na Yesu Kristo kama unavyofafanuliwa katika Agano Jipya. Ni zawadi kubwa kwa Jumuiya ya Kimataifa kuendelea kusimama kidete kulinda na kutetea amani duniani mintarafu haki msingi, utu na heshima ya binadamu hasa katika ulimwengu wautandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia, pengine hata kuliko ilivyokuwa miaka hamsini iliyopita.

Hii ni changamoto ambayo imetolewa hivi karibuni na Kardinali Peter Turkson, Rais wa Baraza la Kipapa la haki na amani wakati alipokuwa anashiriki kwenye Kongamano la Jubilee ya Miaka 50 ya Waraka wa Kichungaji, Amani Duniani, lililofanyika Jimboni Bergamo, Kaskazini mwa Italia. Hii ni changamoto endelevu hata kwa wakati huu ambapo Jumuiya ya Kimataifa inaalikwa kushikamana katika mapambano dhidi ya njaa, umaskini na magonjwa, kwa kuwajengea uwezo wahusika ili waweze kuwajibika barabara kuleta mabadiliko katika maisha na vipaumbele vyao.

Jambo hili linahitaji mikakati na sera makini zinazojikita katika elimu kwani elimu ni mkombozi anayemwezesha mwanadamu kujitegemea na kuyaongoza maisha yake. Watu katika ujumla wao, wanahitaji amani, usalama na maendeleo endelevu. Haya ni mambo ambayo Waraka wa Amani Duniani unayachambua kwa umahiri mkubwa kwa kuikumbatia Familia yote ya binadamu.

Kardinali Turkson anasema kwamba, haya ni matunda ya changamoto zilizotolewa na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, kwa kulitaka Kanisa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa Kristo na Mafundisho yake ili kujenga misingi ya haki, amani, umoja na mshikamano, daima wakitafuta mafao ya wengi. Kanisa linawajibu pia wa kuwajengea watu matumaini yanayobubujika kutoka kwa Mwenyezi Mungu na Amri zake ambazo zinamwelekeo kwa Mungu na binadamu. Demokrasia ya kweli inajengeka kwa kuheshimiana na kusikilizana.

Kardinali Turkson anasema, amani ni zawadi kutoka kwa mwenyezi Mungu inayomshikirisha mwanadamu na kwamba, amani ni utimilifu wa ukweli wote ambao ni Mungu mwenyewe. Matunda ya amani ni: utulivu, furaha na maendeleo endelevu na wokovu wa binadamu. Amani ni zawadi inayomdhihirishia mwanadamu kwamba, anapendwa na kuthaminiwa na Mwenyezi Mungu na inawezekana kupatikana ikiwa kama mwanadamu atakubali kutekeleza mapenzi ya Mungu katika maisha yake.

Utu na heshima ya mwanadamu ni kiini cha mpango wa ukombozi ambao Mwenyezi Mungu ameutekeleza katika historia ya ukombozi, changamoto kwa kila mwamini na wote wenye mapenzi mema kuhakikisha kwamba, amani inatawala duniani. Binadamu na maendeleo yake ni kiini cha Waraka wa Amani Duniani, ili kuleta uwiano mpana kati ya haki na uhuru kama ilivyojitokeza wakati wa vita baridi kati ya mataifa makubwa duniani.

Hata leo hii kuna kinzani zinazoendelea kujitokeza katika Jumuiya ya Kimataifa, mambo yanayotishia amani na utulivu duniani. Maendeleo ya sayansi na teknolojia ya habari yenye uzuri na madhara yake; huduma, ugunduzi, uchafuzi wa mazingira, vitega uchumi, magonjwa, wakimbizi, mitindo ya maisha ni mambo yanayomhitaji kila mtu kuwa ni mjenzi wa amani. Mwanadamu ameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu, akiwa na haki na wajibu anaopaswa kuutekeleza katika Jamii.

Watu wana hamu ya kusikia na kuona ukweli, haki, amani na uhuru; mambo ambayo Baba Mtakatifu Yohane wa ishirini na tatu aliyafafanua kwa kina na mapana katika Waraka wake wa kichungaji, Amani Duniani. Ili kujenga amani ya kweli kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kuzingatia haki msingi za binadamu na kutafuta mambo msingi daima wakiwa wanajizatiti kwa vyombo vya ujenzi wa amani. Baba Mtakatifu Francisko anasema, Kanisa linapaswa kuwa ni chombo cha: haki, amani, matumaini, mapendo na furaha.

Ni matumaini ya Papa Francisko kwamba, Kanisa litaendelea kuwa ni daraja kati ya Mungu na binadamu; litasaidia kuhamasisha utamaduni wa majadiliano ya ukweli na udugu na kwa namna ya pekee miongoni mwa Wakristo na Waislam ili kujenga amani ya kudumu duniani wakiheshimiana na kuthaminiana katika utofauti wao ambao ni utajiri mkubwa kwa Jumuiya ya binadamu.

Imehaririwa na Padre Richard Mjigwa, C.PP.S








All the contents on this site are copyrighted ©.