Papa Francisko akutana na kuzungumza na Rais wa Lebanon na ujumbe wake!
Rais Michel Sleiman wa Lebanon na ujumbe wake, Ijumaa tarehe 3 Mei 2013 amekutana
na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko pamoja na viongozi waandamizi wa Vatican
chini ya uongozi wa Kardinali Tarcisio Bertone, Katibu mkuu wa Vatican.
Viongozi
hawa wawili pamoja na mambo mengine, wamekazia umuhimu wa ujenzi wa utamaduni wa majadiliano
na ushirikiano kati ya Jumuiya ambazo zinatofautiana kikabila na kidini, ambao kimsingi
ni utajiri unaojenga Jamii ambayo inapaswa kujikita kutafuta mafao ya wengi, maendeleo
na utulivu wa taifa. Kuna haja kwa Seikali ya Lebanon kuunda Serikali mpya itakayopewa
dhamana ya kukabiliana na changamoto zinazoendelea kujitokeza kitaifa na kimataifa.
Baba
Mtakatifu Francisko pamoja na Rais Michel Sleiman wamejadili pia kuhusu kinzani na
mgogoro wa kivita unaoendelea nchini Syria; hali ya wakimbizi wanaoendelea kufurika
nchini Lebanon pamoja na nchi jirani; watu ambao kwa sasa wanahitaji msaada wa kiutu,
huku wakiungwa mkono na Jumuiya ya Kimataifa. Wameunga mkono utashi wa kisiasa unaopania
kuanzisha tena mchakato wa mazungumzo kati ya Israeli na Palestina kama njia ya kujenga
na kudumisha amani na utulivu katika Ukanda wa Mashariki ya Kati.
Viongozi
hawa wawili kwa pamoja wameangalia pia hali ya Wakristo ilivyo huko Mashariki ya Kati
pamoja na mchango wa Kanisa mintarafu Waraka wa Kichungaji uliotolewa na Baba Mtakatifu
mstaafu Benedikto wa kumi na sita, Kanisa Mashariki ya Kati, ambao kwa sasa ni Waraka
rejea kwa Jumuiya za Kikatoliki na Jamii mbali mbali huko Mashariki ya Kati.