Mchango wa waamini walei katika kuyatakatifuza malimwengu!
Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi tarehe 4 Mei 2013 anatarajiwa kuongoza Ibada ya
Rozari Takatifu kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria Mkuu lililoko mjini Roma kuanzia
majira ya saa 12:00 Jioni. Jumapili asubuhi ataungana na mashirika ya kitume na vyama
vya sala kutoka sehemu mbali mbali za dunia walioko hapa Roma kwa ajili ya Maadhimisho
ya Mwaka wa Imani.
Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita katika
Waraka wake wa kichungaji, Afrcae Munus, Dhamana ya Afrika anabainisha kwamba, kwa
njia ya waamini walei, Kanisa limo na linafanya kazi ulimwenguni. Waamini walei wanapaswa
kupewa majiundo makini ya maisha ya Kikristo; Kibiblia, Kiroho, Kiliturujia na Kichungaji,
ili waweze kweli kuyatakatifuza malimwengu kwa njia ya maisha na utume wao.
Waamini
walei wanaitwa kwa namna ya pekee kuwa ni watakatifu, ili waweze kuwa kweli ni chumvi
ya dunia na nuru ya ulimwengu. Vyama vya kitume ni majukwaa makini katika mchakato
wa kumshuhudia Kristo ulimwenguni. Waamini Walei wanachangamotishwa kujivunia Ukristo
wao kwa kutambua mchango wanaoweza kuutoa kwa ajili ya mafao ya wengi na maendeleo
endelevu ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.