2013-05-02 08:50:52

Haki msingi za wageni na wahamiaji zinapaswa kulindwa na kuheshimiwa!


Askofu mkuu Francis Assisi Chullikatt, Mwakilishi wa kudumu wa Vatican kwenye Umoja wa Mataifa hivi karibuni ameshiriki katika mkutano wa 46 wa Tume ya Idadi ya Watu na Maendeleo ya Umoja wa Mataifa uliofanyika kwenye Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York, Marekani.

Akichangia mawazo yake anasema kwamba, kuna haja kwa Askari wanaolinda usalama mipakani kutekeleza wajibu wa kazi zao kwa kuongozwa na haki na huruma na kamwe wasiwanyanyase watu wanaovuka mipaka kana kwamba, ni wezi, wanyang'anyi na wavunja sheria, kiasi cha kuonekana kwamba, hawatakiwi ndani ya Jamii.

Jeshi la Polisi mipakani linapaswa kuzingatia sheria za nchi pamoja na haki msingi za wageni, wahamiaji na wakimbizi ambao wakati mwingine wanatafuta hifadhi ya maisha yao.

Kwanza kabisa anasema Askofu mkuu Chullikatt, watu hawa wana haki ya maisha, kupata maendeleo, elimu, mavazi, chakula, malazi na huduma msingi za afya. Hali kwa sasa inaonesha kwamba, wahamiaji wengi wanakabiliana na hali ngumu ya maisha, kwa kutengana na familia zao, kiasi kwamba, watoto wa wahamiaji wanakabiliwa na hali ngumu ya maisha na wakati mwingine wahamiaji hawa wanafanyishwa kazi za suluba; mambo yanayodhalilisha utu na heshima yao kama binadamu walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.

Wanawake wahamiaji wanakabiliwa na hali ngumu zaidi kwani hawa mara nyingi wamekumbana na biashara haramu ya binadamu, nyanyaso na dhuluma za kijinsia. Wahamiaji kama alivyowahi kusema Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Maadhimisho ya Jumapili ya Matawi kwamba, hawa ni wale ambao "si mali kitu mbele ya uso wa mataifa". Lakini utu na heshima yao kama binadamu inawataka wahusika kuhakikisha kwamba, haki zao msingi zinathanimiwa na wote, kwani ni watu wanaokabiliana na changamoto na ugumu wa maisha, kumbe wanapaswa kusaidiwa.

Jumuiya ya Kimataifa anasema Askofu mkuu Chullikatt inapaswa kujenga na kuimarisha mshikamano wa udugu na ushirikiano wa kimataifa ili kuchukua hatua madhubuti zitakazosaidia kuwalinda wahamiaji pamoja na familia zao. Wahamiaji ni watu wenye ujasiri na moyo mkuu, wanaopania kwa namna ya pekee kubadilisha hali ya maisha yao na yale ya ndugu zao kule wanakotoka.

Ni watu ambao wamesaidia pia katika mchakato wa kuimarisha uchumi wa nchi zinazotoa hifadhi pamoja na kuendelea kushirikisha utajiri wa tamaduni na tunu msingi wanazoambatana nazo katika hija ya maisha yao wanapokuwa ugenini. Umoja wa Mataifa unaonesha kwamba, katika kipindi cha miaka ishirini iliyopita, idadi ya wahamiaji duniani imeongezeka na kufikia millioni 60, wengi wao ni wale wanaotoka katika nchi changa zaidi duniani. Hali hii imesaidia pia ongezeko la idadi ya watu wanaozaliwa katika nchi zilizoendelea zaidi duniani. Mchango huu unapaswa kuheshimiwa na kutambuliwa mintarafu sheria za nchi husika.

Ujumbe wa Vatican kwenye mkutano huu, kwa mara nyingine tena uliotoa changamoto kwa Jumuiya ya Kimataifa kulinda na kudumisha haki msingi za wahamiaji kadiri ya Tamko la haki za binadamu lililotolewa na Umoja wa Mataifa.







All the contents on this site are copyrighted ©.