2013-05-02 07:36:32

Bila imani Kanisa litaonekana kuwa kama dala dala iliyokatika usukani!


Maadhimisho ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, miaka hamsini iliyopita, lilikuwa ni tukio kubwa katika maisha na utume wa Kanisa; tukio ambalo liliibua udadisi mkubwa kutoka kwa Wakristo na watu mbali mbali waliokuwa wanafuatilia maisha na utume wa Kanisa kwa wakati huo. Kila mtu alikuwa na matumaini pamoja na wasi wasi ambao ungeweza kuibuliwa na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican. RealAudioMP3
Yote haya yamepita na watu wanazidi kusonga mbele, kiasi kwamba, hata kizazi cha wakati huu kina wasi wasi, matarajio yake. Lakini, jambo la msingi ambalo linapaswa kukumbukwa daima ni changamoto iliyotolewa na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican iliyowataka waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kusoma alama za nyakati, ili kuweza kutenda kadiri ya matarajio na wasi wasi za watu. Mtaguso mkuu ilikuwa ni fursa kwa Kanisa kuweza kupembua alama za nyakati ili kuwajengea watu matumaini kwa njia ya ushuhuda kwa Yesu Kristo Mkombozi wa Ulimwengu.
Ni sehemu ya tafakari ya kina iliyotolewa na Kardinali Zenon Grocholewski, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Elimu Katoliki wakati alipokuwa anashiriki kwenye Kongamano la Kimataifa kuhusu Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican lililokuwa limeandaliwa na Taasisi ya Kipapa ya Dharmaram Vidya Kshetram, Bangalore, India, kama sehemu ya kumbu kumbu ya Maadhimisho ya Jubilee ya miaka 50 ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican. Anasema, furaha, mateso, mahangaiko, matumaini na vipaumbele vya watu ni sehemu ya maisha na utume wa Mama Kanisa ulimwenguni, kwa sababu Kanisa linafanya hija ya maisha na binadamu hatua kwa hatua.
Kanisa linaendelea kuwatia shime binadamu kutoogopa wala kukata tama, kama Yesu alivyowaambia mitume wake, walipomwona akitembea juu ya Bahari, wakashikwa na mshangao mkubwa. Waamini hawana sababu ya kuogopa magumu na vitisho vya dunia hii, bali wanapaswa kusimama kidete kwa kujishikamanisha na Kristo, ili waendelee kuwa kweli ni mashahidi wa matumaini kwa wote waliokata tamaa ya maisha! Kanisa liwaoneshe watu mwanga wa tunu msingi za maisha adili.
Ilikuwa ni hamu ya Papa Yohane wa ishirini na tatu kuhakikisha kwamba, Kanisa linatoa mafundisho ambayo kwa hakika yanagusa undani wa mwanadamu: kiroho na kimwili; kila mtu akijitahidi kutekeleza wajibu na dhamana yake ndani ya Kanisa na Jamii kwa ujumla. Haki, amani, upendo na mshikamano ziwe ni silaha za ujenzi wa Ufalme wa Mungu hapa duniani.
Kwa njia ya kweli za Kiinjili ambazo ni urithi mkubwa wa Mama Kanisa, basi liwasaidie walimwengu kutambua na kuzimwilisha tunu hizi katika medani mbali mbali za maisha. Waamini wanahamasishwa kwenda sehemu mbali mbali za dunia, ili kutangaza Habari Njema ya Wokovu. Sinodi zilizofuatia mara baada ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican anasema Kardinali Grocholewski, zimeendelea kufafanua Utajiri, Mapokeo na Mafundisho Tanzu ya Kanisa, ili yaweze kufahamika kwa waamini na watu wenye mapenzi mema, kama sehemu ya mchakato wa kuyatakatifuza malimwengu.
Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, wakati huo akiwa ni kati ya wataalam wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican anasema kwamba, wajumbe wa Mabaraza ya Maaskofu Katoliki kutoka sehemu mbali mbali za dunia walifika wakiwa na mawazo yao na yale ambayo walipenda Kanisa liyapatie kipaumbele cha kwanza. Lakini, kwa bahati njema, wote walijikuta wakiwa darasani ili kujifunza kile ambacho Roho Mtakatifu alikuwa anawataka kutenda kwa ajili ya Kanisa na Ulimwengu kwa ujumla, wakijikita zaidi na zaidi katika kuleta mabadiliko ya dhati kwa kusoma alama za nyakati.
Walitambua kwamba, Kanisa ni moja; Takatifu, Katoliki na la Mitume. Lina Mapokeo na Urithi ambao unapaswa kuendelezwa na wala hakuna sababu ya kujitenga na Mapokeo ambayo Kanisa limeyasimamia tangu kuanzishwa kwake. Bila Imani, Kanisa lingeonekana kuwa kama “daladala iliyokatika usukani au chumvi ambayo imekosa ladha. Hii ni changamoto ya kuendelea kutoa ushuhuda wa imani tendaji ambayo Kanisa limepokea kutoka kwa Kristo na kuirithisha kwa watu wa vizazi vyote.
Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, wakasiamam imara kutangaza: Mafundisho ya Kanisa katika nyanja mbali mbali, wakionesha pia uhuru wa Kanisa, ili kuwasaidia Walimwengu kutembea katika mwanga wa imani, matumaini na mapendo. Kwa maneno haya Kardinali Zenon Grocholewski amehitimisha mchango wake katika Kongamano la Kumbu kumbu ya Jubilee ya Miaka 50 ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.