Askofu msaidizi Titus Joseph Mdoe umeteuliwa na Mwenyezi Mungu kwa ajili ya kazi yake,
nenda sasa wakati ni huu!
Kardinali Polycarp Pengo, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam, tarehe Mosi,
Mei 2013 amemweka wakfu Askofu msaidizi Titus Joseph Mdoe wa Jimbo kuu la Dar es Salaam
katika Ibada ya misa iliyofanyika kwenye Viwanja wa Msimbazi.
Katika mahubiri
yake Kardinali Polycarp Pengo, amesmhukuru kwa dhati Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto
wa kumi na sita aliyemteua Padre Mdoe kuwa Askofu msaidizi wa Jimbo kuu la Dar es
Salaam. Huu ni upendo ambao ameuonesha kwa namna ya pekee kwa Kanisa la Tanzania,
kama alivyowahi kulipatia Jimbo kuu la Dar es Salaam maaskofu wasaidizi wawili kwa
mara moja.
Baadaye akamteua mmoja wao na kumfanya kuwa Askofu wa Jimbo Jipya
la Ifakara. Kabla ya kung’atuka kutoka madarakani amelipatia tena Jimbo kuu la Dar
es Salaam, Askofu msaidizi ambaye ataendeleza kazi ya kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza
watu wa Mungu.
Kardinali Pengo amesisitiza kwamba jambo la kwanza kabisa
ambalo Askofu anapaswa kutambua ni kuwa uaskofu ni utumishi na wala si madaraka. Akiongelea
kuhusu askofu mteule alimwambia kuwa Mungu amemteua kulichunga kundi lake si kwa sababu
ya mastahili aliyo nayo bali ni kutokana na malengo ya Mungu mwenyewe.
Ameendelea
kwa kusema kwamba, labda kuna watu ambao wanajisikia kufaa zaidi kushika wadhifa huo
labda kwa sababu ni wakubwa zaidi na kimaumbile wanaonekana kama ndo wanaostahili
zaidi; au pia kwa sababu wanayo elimu ya juu zaidi.. mambo yote haya, anasema kardinali,
si maswali ambayo askofu Mdoe anapaswa kuyatafutia majibu.
Mwenyezi Mungu
ana sababu zake zinazokwenda mbali na tofauti kabisa na mawazo hayo hasi ya kibinadamu.
Kazi ya askofu Mdoe ni utumishi wake kwa watu wa Mungu Jimbo kuu la Dar es Salaam
na mahali popote pale atakapotumwa na Mama Kanisa, ili kuwatangazia maskini habari
njema ya wokovu
Naye Waziri mkuu wa Tanzania Mizengo Pinda akitoa salaam za
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, amempongeza Askofu Mdoe kwa kuteuliwa
na hatimaye kuwekwa wakfu kuwa Askofu msaidizi wa Jimbo kuu la Dar es Salaam. Amemtakia
kheri na Baraka katika maisha na utume wake kama Askofu.
Kwa ujumla, Waziri
mkuu amewasisitizia watanzania kuishi kwa upendo na uelewano kati yao; na kamwe chuki
za kidini na kikabila zisikubalike katika jamii kwani haya ni mambo yanayohatarisha
amani ya nchi ya watanzania kwa ujumla wao!. Watanzania wanapaswa kuheshimiana na
kuthaminiana katika utofauti wa dini zao.
Vile vile amewashukuru viongozi
wa dini kwa kuwa daima mstari wa mbele kutafuta yale yanayoleta umoja na mshikamano,
na amewaomba viongozi hao, kuendelea kuwahimiza waamini wao umuhimu wa kuishi katika
amani na kuheshimiana katika toufauti zao hasa zile za kidini, yote hayo yafanyike
kwa nia njema ya kutafuta mafao ya wengi na maendeleo endelevu kwa watanzania wote.
Ibada
hii ya Misa takatifu imehudhuriwa na Maaskofu wa Majimbo Katoliki Tanzania pamoja
na viongozi wa kidini na kiserikali.