Vatican yatuma salam za pongezi kwa Waziri mkuu wa Italia
Kardinali Tarcisio Bertone, Katibu mkuu wa Vatican amemtumia salam za pongezi Waziri
mkuu mpya wa Italia Bwana Enrico Letta kwa kuchaguliwa na hatimaye kupitishwa na Bunge
la Italia. Katika mazungumzo baina ya viongozi hawa wawili kwa njia ya simu, wameweza
kubadilisha mawazo kuhusu baadhi ya vipaumbele vinavyoweza kufanyiwa kazi nchini Italia
na katika ajenda ya Jumuiya ya Ulaya.
Wakati huo huo, Kardinali Angelo Bagnasco,
Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Italia baada ya Maadhimisho ya Misa Takatifu kwenye
Makao makuu ya Benki ya Carige yaliyoko mjini Genova, Siku ya Jumanne tarehe 30 Aprili
2013 amepongeza ziara ya kikazi inayofanywa na Waziri mkuu wa Italia Bwana Enrico
Letta kwamba, inapania kurudisha imani kwa nchi ya Italia ambayo kwa sasa inakabiliwa
na hali ngumu ya uchumi na kuna kundi kubwa la wanawake na vijana hawana fursa za
ajira, jambo ambalo linaendelea kuwakatisha tamaa ya maisha!