2013-05-01 08:04:54

Ushuhuda wa imani katika Familia, sehemu za kazi na kwenye Jumuiya!


Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican katika Maadhimisho ya Mwaka wa Imani, inaendelea kukushirikisha Ujumbe wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania katika kipindi cha Kwaresima kwa Mwaka 2013. Leo tunagusia kuhusu ushuhuda wa imani katika: familia, sehemu za kazi na katika Jumuiya. Kutujuza zaidi ndani ya viunga vya Radio Vatican ni Sr. Gisela Upendo Msuya. RealAudioMP3
Imani ya kweli inapimwa kupitia “afya” ya familia na ya jamii. Haya mawili yanategemeana. Imani isipojidhihirisha katika uhai wa familia, iliyo Kanisa la kwanza, la nyumbani na la msingi, itakuwa ni vigumu kujidhihirisha popote. Familia zetu zinazidi kuwa legelege kwa sababu hazichukuliwi tena kuwa eneo la malezi muhimu ya kiimani na ya kiutu. Malezi ya familia “yamebinafsishwa” katika tendo la kuamini kila mtu katika familia ana wajibu wa kujilea mwenyewe bila ya msaada wa mwingine kati ya wale wanaounda familia moja.
Katika mazingira ya namna hii, dhana nzima ya familia inapotea na familia inapoteza fursa ya kuwa “shule ya imani”, ambamo wazazi na watoto, kwa pamoja, wanakua katika imani. Mwaliko huu wa Mtume Paulo kwa Kanisa la Korintho ni mwaliko kwanza kwa hili “Kanisa la nyumbani”.
Tunazihimiza familia zote za Kikristo kuizingatia imani kwa dhati: Familia, “Simameni imara katika imani”! Ipelekeni nyumbani ile imani mliyoipokea kutoka kwa Mungu kupitia Kanisa lake. Humo mkaiishi na kuijengea mazingira ya kukua. Hili linapotekelezwa, familia itakuwa na uwezo wa kuipeleka imani katika jamii.
“Familia inapata katika mpango wa Mungu Mwumbaji na Mkombozi sio tu utambulisho wake; yaani, yenyewe ni nini, bali pia utume wake; yaani, ni nini inachoweza na inachopaswa kufanya”. Familia zinapoutambua utambulisho wake na utume wake zinaweza kuiishi imani kwa namna bora zaidi. Huo unakua ndiyo mwanzo wa ushuhuda wa kikristo. Ndani ya familia panakuwa ni mahali unamozaliwa moyo wa huruma kwa wanyonge na wasiojiweza. Humo imani inakuwa ni jibu la kutatua hali za kutoelewana katika familia.
Ni kwa namna hii tunaweza kupiga hatua ya kwanza katika kuboresha mazingira ya mahali tunamoishi, kwa sababu “familia ni mahali panapofaa pa kujifunzia na kuzoeshwa utamaduni wa msamaha, amani na upatanisho”. Kwa sababu hiyo wajibu wa malezi endelevu ya imani katika familia unapaswa kuwa wa kudumu. Kwa namna hii tunaweza kuanza kupiga hatua ya kwanza katika kupambana na maradhi hatari kama UKIMWI, kupambana na rushwa, uzembe, na tabia zote ambazo zina athari mbaya kwa makuzi ya mtu binafsi na jamii kwa ujumla. Kwa njia ya imani familia zitapata furaha ya kweli inayojengwa kupitia fadhila za amani na upendo.
Kazini na katika Jumuiya
Mwaliko wa kusimama imara katika imani hauishii kanisani na katika familia tu, ila unaanzia hapo na kutoka hapo mwaliko huu unatekelezwa popote tunapokwenda. “Kukiri kwa mdomo inaonesha kuwa imani inamaanisha ushuhuda na wajibu wa hadharani pia. Mkristo hatakiwi kamwe kufikiri kuwa imani ni tendo la faragha. Imani ni kuchagua kusimama na Bwana ili kuishi naye.” Kuipeleka imani katika jamii ni tendo la ushuhuda wa kikristo. Mtume Yohane anatufundisha kuwa ni kwa njia ya imani tu ndipo tunaweza kuushinda ulimwengu: “Na huku ndiko kuushinda ulimwengu: hiyo imani yetu” (1Yoh 5:4).
Tendo la ushuhuda wa mkristo linalojidhihirisha kwa njia ya imani halina maana ya kujaribu kuwalazimisha watu wengine kuwa wakristo, bali ni kutia katika matendo misingi ya upendo, haki, amani na maelewano kama Kristo anavyotuagiza, na kwa namna hii tunatakatifuza maeneo ya kazi zetu za kila siku na jumuiya zetu. Huku ndiko kuwa chumvi na nuru ya ulimwengu. Na Baba Mtakatifu Benedikto XVI anatuhimiza akisema: “Hatuwezi kukubali chumvi ipoteze ladha au mwanga ubaki umefichwa (rej. Mt 5:13-16).”
Imani ya kweli, ambayo inajidhihirisha katika tendo la waamini kujitoa kama vyombo safi ambavyo Mungu anavitumia kuiumba upya na kuitakatifuza dunia, ni chachu ya kweli kwa mwanadamu na kwa ulimwengu. “Je, si kazi ya Kanisa kutoa mwanga wa Kristo katika kila kipindi cha historia? Si kazi yake kufanya uso wa Kristo ung’are pia mbele ya vizazi vya hii milenia mpya?” Basi, wakati huu wa Kwaresima ni wakati wa kuifanya upya imani yetu kwa njia ya Sakramenti za Kanisa, hasa Sakramenti ya Upatanisho. Vile vile, huu ni wakati wa kufufua matendo ya huruma na upendo na kuyafanya kuwa endelevu katika maisha yetu.
Kanisa hapa nchini linatambua “mchango mkubwa ambao wanawake na wanaume walitoa na kusaidia kukua na kuendelea kwa jumuiya kwa njia ya ushuhuda wa maisha yao.” Baba Mtakatifu Mwenyeheri Yohane Paulo II atabaki kwetu kuwa ni tunda la utakatifu uliojidhirisha katika uaminifu wake kwa Kristo aliyemtanganza na kumtumikia. Maisha yake ya sala, uvumilivu, uongozi wake shupavu na msimamo wake usiotetereka katika kuitafuta na kuikazia macho sura ya Yesu, imemfanya kuwa shahidi wa imani anayepaswa kuwa mfano wa kuigwa.
Wapo pia Watanzania wenzetu ambao maisha yao yalikuwa ni kielelezo cha imani inayojidhihirisha katika matendo. Mtumishi wa Mungu, Mwalimu Julius Nyerere, mwanasiasa mweledi, akiongozwa na dhamiri ya kikristo, ni mmoja wa wakristo waliotukuka katika maisha ya uadilifu wa kisiasa na kiutu.
Mtumishi wa Mungu Sr. Bernadetta Mbawala wa Shirika la Masista Wabenediktini wa Mt. Agnes Chipole, naye alifanikiwa kuitafsiri imani katika maisha yake na hivi akaishi maisha ya upendo unaobubujika kutoka katika imani kwa Mungu na kwa Kanisa. Wakumbukeni hawa na wengine wengi walioishi miongoni mwetu wakimshuhudia Kristo kwa maisha yao, tena, “iigeni imani yao” (Ebr 13:7).








All the contents on this site are copyrighted ©.