Papa mstaafu Benedikto XVI tarehe 2 Mei 2013 anarejea mjini Vatican
Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI anatarajiwa Alhamisi tarehe 2 Mei 2013 majira
ya jioni kurejea mjini Vatican na kuendelea na maisha yake kwenye Konventi ya Mater
Ecclesiae iliyobuniwa na Mwenyeheri Yohane Paulo wa pili kunako mwaka 1989 na kukamilika
kunako mwaka 1992.
Tangu alipong'atuka kutoka madarakani kwa utashi na uhuru
kamili kwa ajili ya mafao na ustawi wa Kanisa amekuwa akiishi kwenye Ikulu Ndogo ya
Castel Gandolfo iliyoko nje kidogo ya mji wa Roma.
Baba Mtakatifu mstaafu
Benedikto XVI wakati wote huu amekuwa akisali na kutafakari kwa ajili ya Kanisa kama
alivyokuwa amesema mwenyewe yapata miezi miwili iliyopita. Padre Federico Lombardi,
msemaji mkuu wa Vatican amethitisha habari hizi na kuongeza kwamba, afya ya Baba Mtakatifu
mstaafu Benedikto wa kumi na sita ni njema, ila tu umri unazidi kumwelemea na kwamba,
amedhohofu kidogo!