Mtu asiyefanya kazi amepoteza utu na heshima yake!
Jamii ambayo haiwezi kutoa fursa ya ajira kwa watu wake na badala yake, inawanyonya
kwa kuwaptia ujira kidogo haiwatendei haki watu wake. Ni sehemu ya mahubiri yaliyotolewa
na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu kwenye
Kikanisa cha Domus Sanctae Marthae kilichoko mjini Vatican, Mei Mosi, 2013, kumbu
kumbu ya Mtakatifu Yosefu Mfanyakazi. Ibada hii imehudhuriwa na wasichana wazazi wanaopewa
hifadhi kwenye Jumuiya ijulikanayo kama "Il Ponte".
Maandiko Matakatifu yanaonesha
kwamba, Mtakatifu Yosefu alikuwa ni Seremala kiasi kwamba, hata Yesu akaitwa ni Mwana
wa Seremala. Mwenyezi Mungu alifanya kazi ya uumbaji kwa siku sita na siku ya saba
akapumzika, kielelezo kwamba, kazi inampatia mwanadamu utu na heshima yake. Inasikitisha
kuona kwamba, watu wanathamini zaidi vitu kuliko hata utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa
kwa sura na mfano wa Mungu. Waajiri wengi wanatafuta faida kubwa hata kwa gharama
ya maisha ya wafanyakazi wao.
Wanasiasa kwa upande wao wanatafuta madaraka
kuliko hata ustawi na maendeleo ya wananchi wanaowaongoza. Baba Mtakatifu anasema
kwamba, kwa mwelekeo kama huu Jamii nyingi zimejikuta zikigonga mwamba kwa kutothamini
utu wa mwanadamu na dhamana ya kazi katika maisha ya watu. Kwa mtu ambaye hana fursa
ya kufanya kazi kwa hakika amepoteza utu na heshima yake.
Huu ni mwaliko kwa
Jamii kuhakikisha kwamba, inaboresha hali ya maisha ya wafanyakazi pamoja na kupambana
kufa na kupona na madhulumu yanayoendelea kufanyika katika maeneo ya kazi.