Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe Mosi, Mei anaadhimisha Kumbu kumbu ya Mtakatifu
Yosefu Mfanyakazi, sanjari na Siku ya Wafanyakazi Duniani. Kanisa linatambua na kuthamini
umuhimu wa kazi kama wajibu na utimilifu wa mwanadamu na ushiriki wake katika kutiisha
dunia pamoja na kutoa huduma kwa Jumuiya ya binadamu.
Mababa wa Mtaguso mkuu
wa pili wa Vatican wanasema, huu ni mwendelezo wa ushiriki wa mwanadamu katika kazi
ya uumbaji na mpango wa ukombozi.
Kumbu kumbu ya Mtakatifu Yosefu msimamizi
wa wafanyakazi, ilianzishwa kunako mwaka 1955 na Baba Mtakatifu Pio wa kumi na mbili.
Akaamuru kwamba, siku hii iadhimishwe sanjari na Siku ya Wafanyakazi Duniani, kila
mwaka ifikapo tarehe Mosi, Mei.