2013-05-01 09:24:16

Angalieni vyema kuhusu matangazo ya biashara yanayopania kupotosha ukweli wa Mafundisho ya Kanisa!


Askofu mkuu Peter Kairo wa Jimbo kuu la Nyeri, Kenya amewataka waamini na watu wenye mapenzi mema nchini Kenya kuwa macho na makini zaidi kwa baadhi ya watu wanaotaka kutumia jina la Kanisa Katoliki kwa ajili ya mafao na masilahi yao binafsi, kiasi hata cha kuchapisha matangazo yanayokwenda kinyume cha maadili na msimamo wa Kanisa Katoliki kuhusu Kondom.

Askofu mkuu Kairo wakati wa mahubiri yake kwenye Parokia ya Kagicha Jimboni humo hivi karibuni amewataka waamini kuwa waaminifu na kuendelea kuishi kadiri ya misingi na kanuni za Kanisa Katoliki mintarafu Maandiko Matakatifu na Mapokeo ya Kanisa, huku wakiheshimiana na kujaliana. Hivi karibuni kwenye vyombo mbali mbali vya habari nchini Kenya vimekuwa vikichapisha matangazo ya biashara "yanayopigia debe" matumizi ya kondomu, kinyume kabisa cha Mafundisho ya Kanisa.

Askofu mkuu Peter Kairo anafafanua kwamba, Kanisa Katoliki linawafundisha waamini wake kutunza usafi wa moyo, kuwa waaminifu kwa wenzi wao wa ndoa na kujizuia. Wanandoa wanapaswa kujenga na kuimarisha utamaduni wa kuheshimiana katika maisha ya ndoa na familia. Hili ni jukumu ambalo pia linapaswa kufanyiwa kazi na vijana kwa kutambua kwamba, dunia ya leo ni tambara bovu wasipokuwa makini na matangazo ya biashara, wanaweza kujikuta wanatumbukizwa pabaya.







All the contents on this site are copyrighted ©.