Weekeni mikakati na sera makini kuzuia magonjwa na ajali kazini
Taarifa ya Shirika la Kazi Duniani, ILO inaonesha kwamba, kila mwaka kuna watu zaidi
ya millioni mbili duniani wanaofariki dunia kutokana na magonjwa wanayoyapata wakiwa
kazini. Idadi hii ni kubwa zaidi kuliko hata ile ya watu wanaofariki dunia kutokana
na ajali barabarani. Itakumbukwa kwamba, Jumuiya ya Kimataifa, hapo tarehe 28 Aprili
2013 imeadhimisha Siku ya Afya na Usalama Kazini.
Kumekuwepo na ajali nyingi
kazini ambazo zinapelekea vifo vya wafanyakazi. Shirika la Kazi Duniani linakadiria
kwamba, kila mwaka walau kuna wafanyakazi zaidi ya millioni 160 wanaoambukizwa magonjwa
wakiwa kazini. Hii inatokana na ukweli kwamba, watu wengi wanafanya kazi katika mazingira
duni hata pengine kinyume cha utu na heshima ya binadamu. Magonjwa kazini hayajapata
kipaumbele cha kutosha kiasi kwamba, watu wanaendelea kupoteza maisha kila siku, jambo
ambalo kamwe haliwezi kuvumiliwa.
Kuna haja ya Serikali na sekta binafsi kujipanga
kwa kuibua mbinu mkakati zitakazosaidia kuzuia magonjwa na ajali kazini. Kuna mamillioni
ya wafanyakazi ambao maisha yao yako hatarini, kumbe hili si jambo la kupuuziwa bali
linapaswa kuwekewa mikakati madhubuti sanjari na kuzuia ajali kazini. Hali hii pia
inachangia kwa namna ya pekee katika kuzorota kwa uchumi pamoja kuendelea kupukutisha
nguvu kazi ambayo ingetumika kwa ajili ya uzalishaji na utoaji wa huduma.