Utu na heshima ya mwanadamu ni kipimo tosha kabisa cha heshima ya kazi!
Tarehe Mosi, Mei, wafanyakazi sehemu mbali mbali za dunia wanaadhimisha Siku yao sanjari
na Siku kuu ya Mtakatifu Yosefu mfanyakazi aliyejitaabisha kuhakikisha kwamba, Familia
Takatifu inapata mahitaji yake msingi. Kutokana na umakini wake katika masuala ya
kazi, Kanisa limemweka Mtakatifu Yosefu kuwa ni msimamizi wa Wafanyakazi kwani linatambua
kwamba, utu wa mwanadamu ndicho kipimo cha heshima ya kazi. Hii ndiyo thamani kubwa
ya kazi kiimadili.
Kazi ni wajibu
na utambulisho wa mwanadamu na kwamba, nguvu kazi inapaswa kupewa kipaumbele cha pekee.
Kuna uhusiano wa pekee kati ya nguvu kazi na mtaji. Jambo hili linaweza kueleweka
zaidi ikiwa kama wafanyakazi wanashiriki katika umiliki, usimamizi na faida. Kwa
muhtasari haya ni kati ya mambo yanayotiliwa mkazo katika mfaundisho Jamii ya Kanisa
kuhusiana na dhana ya kazi.
Baraza la Maaskofu Katoliki Canada katika Maadhimisho
ya Siku ya Wafanyakazi Duniani hapo tarehe Mosi, Mei, 2013, linawaalika wafanyakazi
na watu wenye mapenzi mema kuhakikisha kwamba, katika maandamano, semina, makongamano
na mikutano watakayofanya kama sehemu ya Maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani
wajitahidi kuweka ladha ya imani katika matukio yote haya, ili kuamsha hisia ya utajiri
na rasilimali ya nchi kugawanywa katika mizani sawa pamoja na kuishirikisha Jamii
katika mikakati na sera za maendeleo ya nchi.
Maaskofu wanawataka wafanyakazi
kusimama kidete kupinga mabadiliko yatakayokuwa na athari kubwa katika maisha ya wafanyakazi
na familia zao nchini Canada. Kuna haja kufanya mabadiliko ya dhati katika mifumo
ya uchumi na mashirika na taasisi za fedha ambayo kwa sasa kutokana na ukiritimba
na sera tenge yamepelekea wafanyakazi wengi kukosa fursa za ajira na hivyo kujikuta
wanatumbukia katika dimbwi la umaskini wa kipato, kihali na maisha ya kiroho.
Baraza
la Maaskofu Katoliki Canada linaonesha uhusiano wa dhati kati ya imani na mshikamano
wa upendo na udugu unaopaswa kuoneshwa miongoni mwa wafanyakazi, kwa kuonesha mantiki
mpya inayojikita katika mshikamano wa upendo unaovuka ubinafsi na hivyo kuwafanya
waweze kusaidiana kwa hali na mali. Ni mshikamano unaopania kukuza na kumwendeleza
mtu mzima: kiroho na kimwili; kwa kutafuta mafao ya wengi, huku wakijitahidi kulinda
na kutunza mazingira ambayo kimsingi ni sehemu ya kazi ya uumbaji.
Baraza la
Maaskofu Katoliki Canada linahitimisha ujumbe wake katika Maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi
Duniani, kwa kuwataka wafanyakazi kuonesha mshikamano ili kujenga na kuimarisha utawala
wa sheria unaosimikwa katika maadili na utu wema, kuanzia katika ngazi ya kitaifa
hadi kimataifa. Lengo ni kuendeleza demokrasia ya kweli na haki. Maaskofu wanawatakia
wafanyakazi wote: furaha, amani na utulivu wanaposherehekea Siku ya Wafanyakazi Duniani
kwa Mwaka 2013.