2013-04-30 14:37:39

Rais Shimon Perez akutana na Papa Francisko mjini Vatican


Baba Mtakatifu Francisko, Jumanne, tarehe 30 Aprili 2013 amekutana na kufanya mazungumzo na Rais Shimon Peres wa Israeli, ambaye baadaye pia amekutana na ujumbe wa Viongozi waandamizi kutoka Vatican wakiongozwa na Kardinali Tarcisio Bertone, Katibu mkuu wa Vatican.

Katika mazungumzo haya ambayo yamefanyika katika hali ya kirafiki, amani na utulivu mkubwa, viongozi hao wamejadili kuhusu hali ya kisiasa huko Mashariki ya Kati na sehemu nyingine za dunia ambako bado kuna kinzani na migogoro ya kisiasa na kijamii. Viongozi hawa wanatumaini kwamba, majadiliano kati ya Israeli na Palestina yataanza mapema iwezekanavyo kama inavyokusudiwa kwa kuchukua hatua madhubuti, huku wakiungwa mkono na Jumuiya ya Kimataifa; ili hatimaye, makubaliano yaweze kufikiwa baina ya watu wa mataifa haya mawili, ili amani na utulivu viweze kurejea tena katika Ukanda huo.

Baba Mtakatifu pamoja na mgeni wake wamejadili pia kuhusu Mji wa Yerusalemu; kinzani na vita inayoendelea huko Syria na kwamba, kuna haja ya kukazia utamaduni wa: majadiliano, upatanisho, haki na amani. Uhusiano kati ya Vatican na Israeli, pamoja na Jumuiya za Kikristo nchini Israeli yamejadiliwa pia pamoja na kuangalia Tume ya pamoja kati ya Israeli na Vatican na kuangalia mafanikio ambayo yamekwisha kupatikana hadi sasa.







All the contents on this site are copyrighted ©.