Majadiliano ya kidini ni sehemu ya mchakato wa Uinjilishaji mpya!
Vijana wa Kiislam na Kikristo wanakabiliana na changamoto kubwa katika ujenzi wa misingi
ya haki, amani na utulivu katika jamii zao hasa wakati huu ambapo Jumuiya ya Kimataifa
inashuhudia kwa kiasi kikubwa athari za myumbo wa uchumi kimataifa. Jamii nyingi zinakabiliwa
pia na athari za mmong’onyoko wa kimaadili na kiutu, mambo ambayo yanatikisa msingi
ya maisha na utume wa Familia. Vijana wanatafuta utambulisho wao wa kidini katika
ulimwengu mamboleo.
Hizi ni changamoto zinazofanyiwa kazi na Wawakilishi kutoka
Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Barani Ulaya, kuanzia tarehe Mosi, Mei
hadi tarehe 3 Mei, 2013 Jijini London. Ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi
na teknolojia unaendelea kutoa changamoto mpya kwa Kanisa, kiasi kwamba, majadiliano
ya kidini na waamini wa dini ya Kiislam ni jambo ambalo linapaswa kupewa msukumo wa
pekee, ili kujenga na kuimarisha: misingi ya haki, amani, upendo mshikamano na utulivu.
Majadiliano ya kidini ni sehemu ya mchakato wa Uinjilishaji mpya unaofanywa
na Mama Kanisa katika mapambazuko ya Millenia ya Tatu ya Ukristo. Waamini wanatumwa
kumtangaza Kristo mkombozi wa ulimwengu; wakiheshimu na kuthamini uhuru wa kidini,
kila mtu akiwa huru kutolea ushuhuda wa imani yake bila kificho.
Mkutano wa
wawakilishi wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Barani Ulaya unaongozwa
na kauli mbiu “Majadiliano na Utangazaji wa Habari Njema ya Wokovu”, unaratibiwa na
Kardinali Jean Pierre Ricard, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Bordeaux.
Viongozi
wengine wanaoshiriki ni pamoja Askofu mkuu Vincent Nichols, Rais wa Baraza la Maaskofu
Katoliki Uingereza. Kardinali Jean Louis Tauran, Rais wa Baraza la Kipapa la Majadiliano
ya Kidini ndiye anayefungua mkutano huu. Majadiliano na Uinjilishaji ni mada ambazo
ziliwahi kujadiliwa kwa kina na mapana kunako mwaka 1991.
Katika mkutano huu,
wajumbe watapata fursa ya kubadilishana mawazo, mang’amuzi pamoja na changamoto mbali
mbali wanazokabiliana nazo katika maisha na utume wa Kanisa huko waliko. Umuhimu wa
ujenzi wa utambulisho wa vijana kidini ni mada inayopembuliwa kwa mapana na marefu
pamoja na kuangalia hali ya maisha ya Waamini wa dini ya Kiislam kutoka katika nchi
mbali mbali za Ulaya mintarafu uhusiano na Wakristo.