Kanisa Katoliki nchini Ireland, Jumamosi tarehe 4 Mei 2013 linaadhimisha Siku ya kuenzi
zawadi ya uhai inayopania kuwahamasisha waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kusimama
kidete kulinda na kutetea zawadi ya maisha tangu pale mtoto anapokuwa bado tumboni
mwa mama yake dhidi ya utamaduni wa kifo.
Kauli mbiu ya Maadhimisho kwa Mwaka
2013 ni "tumbo kwa tumbo". Kitaifa siku hii itaadhimishwa kwenye Kanisa la Bikira
Maria wa Knock kwa kuwashirikisha waamini na watu wote wenye mapenzi mema kutoka Majimbo
mbali mbali ya Ireland, ili kuombea haki ya maisha kwa watoto ambao bado hawajazaliwa;
watoto ambao wanatishiwa na ukatili wa utamaduni wa kifo.
Kutokana na Serikali
ya Ireland kukumbatia sheria inayoruhusu utoaji mimba, wanasema Maaskofu, watoto wengi
nchini humo watakosa haki ya kuweza kuishi na kufurahia maisha ambayo kimsingi ni
zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Kwa kuchagua kuenzi na kusimama kidete kulinda na
kutetea zawadi ya maisha, mama na mwana wote wawili wanapewa kipaumbele cha pekee.
Siku hii imetengwa na Kanisa kwa ajili ya kuwakumbuka na kuwaombea akina mama
na watoto wao, ili kweli wawe ni vyombo vya kuenzi zawadi ya uhai. Kanisa linawaombea
ili kuwaepusha na kila ubaya; waendelee kupendwa na kuthaminiwa na wote.
Baraza
la Maaskofu Katoliki Ireland linawaalika wanafamilia wote kushiriki kikamilifu katika
Maadhimisho ya Siku hii maalum kwa ajili ya kuenzi zawadi ya uhai dhidi ya utamaduni
wa kifo. Siku hii imekuwa ikiadhimishwa nchini humo tangu mwaka 2001, kama sehemu
ya mchakato wa kuenzi Mafundisho ya Mwenyeheri Yohane Paulo wa pili kuhusu Injili
ya Maisha "Evangelium Vitae". Mwaka 2012 waamini walitafakari kuhusu umuhimu wa mshikamano
na matumaini katika Jamii.