2013-04-30 08:35:13

Kuzeni na kuimarisha fadhila ya unyenyekevu, toba na wongofu wa ndani, ili kuonja huruma na upendo wa Mungu


Sakramenti ya Upatanisho ni mahali ambapo mwamini katika hali ya unyenyekevu na moyo wa toba anakutana na hatimaye, kuonja huruma na upendo wa Mungu kwa njia ya Yesu Kristo. Ni mwaliko na changamoto kwa waamini kuhakikisha kwamba wanaipokea Sakramenti hii kwa kufanya maandalizi ya kina ili kuweza kufaidi neema na baraka zinazotolewa na Mama Kanisa. Fadhila ya unyenyekevu inamwezesha mwamini kutambua kwamba ni mdhambi na anahitaji huruma na upendo wa Mungu.

Hayo yamesemwa na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kikanisa cha Domus Sanctae Mathae kilichoko mjini Vatican, Jumatatu tarehe 29 Aprili 2013 na kuhudhuriwa na na viongozi pamoja na wafanyakazi kadhaa kutoka Vatican. Anasema, mbele ya Mwenyezi Mungu hakuna giza, changamoto kwa waamini kutembea katika njia ya haki na ukweli; ili kuweza kumwabudu Mungu katika roho na ukweli. Kutembea katika giza kuna maanisha kwamba, mwamini ameridhika na hali ya maisha yake na kwamba, hana haja ya kutafuta wokovu na maisha ya uzima wa milele.

Waamini watambue mapungufu yao ya kibinadamu, wawe tayari kufanya toba na kumrudia tena Mwenyezi Mungu, kwani Yeye ni mwingi wa huruma na mapendo wala si mwingi wa hasira, ndiyo maana anataka kumwokoa mwanadamu kwa kumkirimia amani ya ndani. Anatambua yote, daima yuko tayari kumpokea yeyote anayemwendea kwa machozi ya toba, unyenyekevu na ukweli; kwani hizi ni fadhila za kikristo na kiutu.

Baba Mtakatifu anasema, Roho Mtakatifu anawaondolea waamini dhambi zao, pale wanapotubu kutoka katika undani wa mioyo yao; pale wanapoelemewa na mzigo wa dhambi, wasisite kumkimbilia naye atawapumzisha. Sakramenti ya Upatanisho ni mahali pa kumsifu na kumtukuza Mwenyezi Mungu, kwa zawadi ya ukombozi kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Wakristo wakuze na kuimarisha ndani mwao ile fadhila ya unyenyekevu, toba na wongofu wa ndani, ili waweze kuonja huruma na upendo wa Mungu usiokuwa na kifani!







All the contents on this site are copyrighted ©.