2013-04-30 08:51:02

Changamoto katika kudumisha utawala bora!


Utawala bora katika ulimwengu unaobadilika ndiyo kauli mbiu iliyofanyiwa kazi na Baraza la Kipapa la Sayansi Jamii, katika mkutano wake wa mwaka uliohitimishwa hivi karibuni hapa mjini Vatican. Kwa namna ya pekee, wamegusia kumbu kumbu ya Maadhimisho ya Jubilee ya miaka 50 tangu Papa Yohane wa Ishirini na tatu alipochapisha Waraka wa Kichungaji, Pacem in Terris, Amani Duniani. Wajumbe wa Baraza hili wameangalia changamoto zinazoikabili Jumuiya ya Kimataifa katika mchakato wa kuimarisha utawala bora.

Professa Mary Ann Glendon, Rais wa Baraza la Kipapa la Sayansi Jamii katika hotuba yake ya ufunguzi amezungumzia umuhimu wa siasa inayozingatia kanuni maadili katika maisha ya mtu binafsi na jamii inayomzunguka. Uongozi ufahamike kwamba ni uwezo wa kutafuta mafao ya wengi na kwamba, amani ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu inayomshirikisha mwanadamu.

Kardinali Peter Turkson, Rais wa Baraza la Kipapa la haki na amani anabainisha kwamba, utawala bora ni kati ya mambo msingi yanayoiwezesha jamii kupata mafao ya wengi. Ni mwaliko pia wa kufanya toba na kuchuchumilia wongofu wa ndani ili kuweza kukumbatia upendo unaobubujika kutoka kwa Kristo mwenyewe. Watu wakijitahidi kudumisha upendo kati yao, maendeleo yatafuata, kwani amani ni jina jipya la maendeleo endelevu ya binadamu.

Kardinali Turkson anakazia kwamba, dhamana na wajibu wa kujenga na kuimarisha amani ni kwa watu wote wenye mapenzi mema, changamoto kwa kila mtu kujitahidi kuwa ni chombo cha amani na mafao ya wengi. Wajumbe hawa pia walipata bahati ya kukutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko mjini Vatican.







All the contents on this site are copyrighted ©.