2013-04-29 09:50:55

Zaidi ya Makanisa 70 yamechomwa moto nchini Nigeria!


Kinzani za kiuchumi, kijamii, kisiasa na kidini nchini Nigeria, zimepelekea zaidi ya Makanisa 70 kuchomwa motokwenye Jimbo la Benue, Kati kati mwa Nigeria, kiasi kwamba, kuna maelfu ya waamini hasa wale wanaoishi vijijini hawana tena nyumba za Ibada.

Hayo yamo kwenye taarifa kutoka kwenye Tume ya haki, amani na maendeleo ya Jimbo Katoliki Makurdi. Kuna idadi kubwa za shule za msingi na sekondari ambazo zinamilikiwa na Makanisa nchini Nigeria zimechomwa pia moto katika miezi ya hivi karibuni.

Kinzani za kikabilia na kati ya wakulima na wafugaji nchini Nigeria zimepekea maafa makubwa kwa maisha na mali za watu. Mapigano haya wakati mwingine yamekuwa ni makali kutokana na silaha za moto zinazotumika hali ambayo inaonesha kwamba, kuna silaha nyingi ambazo zinamilikiwa kinyume cha sheria za nchi na hivyo kuhatarisha amani na usalama wa wananchi wa Nigeria.

Viongozi wa Makanisa nchini Nigeria wanaitaka Serikali kusimama kidete kulinda na kutetea maisha na mali ya raia wake na kwamba, sheria ichukue mkondo wake kwa wote wanaobainika kwamba, wanaleta vurugu nchini humo.







All the contents on this site are copyrighted ©.