2013-04-29 08:04:18

Wakristo wanahamasishwa kushiriki katika mchakato wa Uinjilishaji Mpya kama njia ya kuyatakatifuza malimwengu!


Kardinali Braz de Aviz, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume, hivi karibuni amehitimisha hija yake ya kichungaji nchini Taiwan na kuwataka waamini kuendelea kuonesha mshikamano wao wa dhati na Baba Mtakatifu Francisko na kila mmoja akitambua na kuendelea kushiriki kikamilifu katika mchakato wa Uinjilishaji mpya, kama njia ya kuyatakatifuza malimwengu. RealAudioMP3

Kardinali Braz de Aviz ameyasema hayo wakati wa maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu, iliyotolewa kwa ajili ya kumwombea Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume wake, ibada ambayo ilihudhuriwa na Familia ya Mungu nchini Taiwan. Akiwa nchini Taiwan, Kardinali Braz de Aviz alipata fursa ya kutembelea, kuzungumza na kubadilishana: mawazo na mang’amuzi mbali mbali na Jumuiya za Watawa wanaoishi na kutekeleza utume wao nchini Taiwan. Alishiriki pia katika mkutano mkuu wa Wakuu wa Mashirika ya Kitawa nchini humo.

Kardinali Braz de Aviz alichangia mawazo kwenye mkutano wa kitaaluma nchini Taiwan uliokuwa unajadili kwa namna ya pekee vielelezo vya umoja: majadiliano mseto kuhusu mawazo ya Chiara Lubich, kama sehemu ya kumbu kumbu ya miaka mitano tangu Chaiara Lubich alipofariki dunia. Mkutano huu umefanyika kwenye Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Fu Jen, huko New Taipei City.

Anasema kati ya zawadi kubwa ambazo Mama Chiara Lubich mwanzilishi wa Chama cha Kitume cha Wafokolare aliyoliachia Kanisa ni umoja unaopaswa kujionesha kwa “Kanisa moja, Takatifu, Katoliki na la Mitume” Huu ndio umoja na mshikamano ambao hata Yesu Kristo mwenyewe aliwaombea wafuasi wake katika ile Sala ya Kikuhani na Baba Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili akaikazia kwa namna ya pekee katika Waraka wake wa Kichungaji, “Ut Unum Sint”, Ili Wawe na Wamoja.

Hii ni changamoto pevu inayopasa kufanyiwa kazi na Mama Kanisa kwa kutambua kwamba, watoto wake wanatoka katika tamaduni, mila na desturi mbali mbali; wakiwa na amana zao za maisha ya kiroho na kitamaduni, lakini wote kwa pamoja wanaalikwa kujenga na kudumisha umoja wa Kanisa la Kristo, kwani yote haya ni utajiri unaopaswa kufanyiwa kazi na Mama Kanisa.

Wakristo bado wanaendeleza mchakato wa umoja kati yao hata katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo, kwani hata sasa bado Kanisa limegawanyika ndiyo maana kuna haja ya kukuza na kuendeleza majadiliano ya Kiekumene, ili wote wawe wamoja.

Jitihada hizi zinakwenda sanjari na majadiliano ya kidini na waamini wa dini nyingine duniani ili kujenga amani, upendo na mshikamano, kwa kutafuta mafao ya wengi, haki na amani. Fumbo la Utatu Mtakatifu liwe ni kielelezo cha umoja unaotafutwa na Mama Kanisa miongoni mwa watoto wake.

Mama Chiara Lubich katika maisha yake alijitoa wakfu kwa maisha ya usafi wa moyo kama njia ya kumtumikia Mungu, akijikita katika mchakato wa kudumisha umoja na mshikamano miongoni mwa Jamii ya watu. Huu ni wito maalum, kwani wengi wamezoea wito wa kitawa, kipadre au maisha ya ndoa. Mama Chiara Lubich alijitahidi kumwilisha ndani mwake ile amri ya upendo kwa Mungu na jirani.

Amri hii inajikita na kujielekeza katika kudumisha na kuimaarisha upendo na watu wenye miito mbali mbali ndani ya Kanisa; upendo ambao kwa namna ya pekee unasaidia utekelezaji wa shughuli na mikakati ya kuchungaji kati ya waamini walei, watawa, vyama vya kitume, taasisi na makundi ya watu. Kardinali Braz de Aviz anasema, changamoto na karama kubwa inayopaswa kufanyiwa kazi kwa sasa ni umoja miongoni mwa wafuasi wa Kristo.








All the contents on this site are copyrighted ©.