Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro wageuka na kuwa kama ile Siku ya Pentekoste!
Askofu mkuu Rino Fisichella Rais wa Baraza la Kipapa la Uhamasishaji wa Uinjilishaji
Mpya akiwatambulisha Wakristo 44 waliopewa Sakramenti ya Kipaimara na Baba Mtakatifu
Francisko kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, alisema, wamesindikizwa
na Wazazi, Mapadre pamoja na Makatekista waliowaandaa kwa ajili ya kupokea Sakramenti
za Kanisa kama sehemu ya Maadhimisho ya Mwaka wa Imani.
Huu ni mwaliko kwa
kila mwamini kukuza na kuimarisha ile Imani aliyopokea wakati wa Sakramenti ya Ubatizo.
Kundi hili la Wakristo 44 linawawakilisha vijana kutoka sehemu mbali mbali za dunia
watakapokea Sakramenti ya Kipaimara wakati wa Maadhimisho ya Mwaka wa Imani. Wao kama
ilivyo kwa waamini wengine, watapokea Mapaji ya Roho Mtakatifu, tayari kwenda sehemu
mbali mbali za dunia, kumshuhudia Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kutoka katika
wafu kama ilivyokuwa Siku ile ya Pentekoste.
Askofu mkuu Rino Fisichella anasema
kwamba, waamini wanaalikwa kwa namna ya pekee kutubu na kuongoka ili kuweza kupokea
Neno la Mungu na neema zake zinazoleta mageuzi na maisha mapya kwa kuwakirimia Mapaji
Saba ya Roho Mtakatifu.
Waamini walioimarishwa kwa Sakramenti ya Kipaimara
wanachangamotishwa na Mama Kanisa kuendelea kufanya hija ya furaha na matumaini kama
alama hai ya upendo na huruma ya Mungu kwa waja wake.