Mawaziri Italia wala kiapo wakati damu ya Askari Polisi ikimwagika nje ya Ikulu!
Baraza la Mawaziri nchini Italia lenye Mawaziri 21, linaloongozwa na Waziri mkuu mpya
Bwana Enrico Letta, Jumapili tarehe 28 Aprili 2013, limekula kiapo cha utii kwa Jamhuri,
wakati ambapo Jeshi la Polisi lilikuwa likipambana na Bwana Luigi Preiti aliyeingia
kwenye eneo la tukio akiwa na lengo la kuwafyatulia risasi wanasiasa lakini kwa bahati
mbaya, risasi hizi zikawapata Askari wawili waliokuwa kwenye ulinzi.
Kati
yao Askari mmoja amefanyiwa upasuaji mkubwa na hali yake bado si nzuri. Viongozi mbali
mbali wa Serikali na Vyama vya Kisiasa nchini Italia vimeshutumu sana kitendo hiki
ambacho kimevuruga amani na utulivu wakati wa sherehe za kula kiapo kwa Baraza la
Mawaziri la Italia.
Kardinali Angelo Bagnasco, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki
Italia anabainisha kwamba, hili ni onyo kwa wanasiasa kwani inaonekana kwamba, watu
wengi wamekata tamaa kutokana na athari za myumbo wa uchumi kimataifa na kwamba, wanasiasa
wanapaswa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa mafao ya wengi badala ya kujitafuta wao
wenyewe na matokeo yake ni vitendo vya kukata tamaa ambavyo wananchi wamekuwa wakivionesha
kwa sasa.