2013-04-27 11:37:55

Muswada wa sheria kuhusu "siri za Serikali" una mapungufu makubwa!


Baraza la Maaskofu Katoliki Afrika ya Kusini limemwomba Rais Jacob Zuma wa Afrika ya Kusini, kupeleka muswada wa sheria ya habari za kitaifa kwenye Mahakama ya Katiba kabla ya kuupitisha na kuwa sheria kamili kutokana na mapungufu makubwa yaliyojionesha kwenye muswada huo. RealAudioMP3

Ushauri huu umetolewa na Askofu mkuu Stephen Brislin, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Afrika ya Kusini. Anasema, Rais Zuma ndiye mwenye mamlaka ya kuweza kuupeleka muswada huo wa sheria kwenye Mahakama ya Katiba ili uweze kuchambuliwa vizuri zaidi kabla ya kuwekwa sahihi na kuwa sheria ya nchi. Hii inatokana na ukweli kwamba, Wabunge wametumia muda mwingi kuufanyia marekebisho lakini bila kupata muafaka kwa takribani miaka mitatu sasa.

Muswada unaonesha kwamba, Serikali inayo mamlaka kudhibiti siri za Serikali, hali ambayo wadau wengi wa mawasiliano ya jamii wanasema, kinaweza kuwa ni kichaka cha kuficha masuala ya rushwa, wizi na ufisadi wa mali ya umma kwa kisingizio cha kuwa ni "siri ya serikali". Mapambano dhidi ya rushwa na ubadhirifu wa mali ya umma yanapaswa kuongozwa na ukweli na uwazi; ujasiri na uwajibikaji kwa ajili ya mafao ya wengi badala ya usiri mkubwa unaoweza kukwamisha mapambano haya.

Hukumu ya miaka 25 kwa watu watakovujisha siri za Serikali ni kubwa mno kiasi kwamba, watu wanaotaka kukwamisha mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi wanaweza kuitumia sheria hii kwa mafao ya binafsi. Wananchi wa Afrika ya Kusini wanahitaji kuwa na uhuru wa habari.







All the contents on this site are copyrighted ©.