2013-04-26 07:47:11

Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya tano ya Kipindi cha Pasaka


Mpendwa mwana wa Mungu, tunaendelea katika furaha ileile ya Pasaka, na katika Dominika hii ya 5 ya Pasaka mwaka C tunatafakari upendo wa Mungu ambao watujia kwa njia ya amri mpya, ambayo yaumba dunia mpya na jumuiya mpya. RealAudioMP3

Mwinjili Yohane akinukuu maneno ya Bwana anasema pendaneni kama nilivyowapenda ninyi, na kwa namna hiyo watu wote watatambua kuwa ninyi ni wafuasi wangu. Kumbe sasa ndugu yangu mpendwa ujumbe uko wazi, wajibu ni kuuweka katika matendo yako yak ila siku ukiendelea kusaidiwa na Neno la Mungu.

Katika mantiki ya kila siku ya maisha ya kiimani, ukristu ni UMOJA na hivi si kitu cha mtu mmojammoja na hivyo, tunaalikwa kuishi maisha ya jumuiya mpya. Katika hili tunamwona Mt Paulo na Mt Barnaba wakiwa maisha mfano, wanapita katika jumuiya walizozianzisha, wakisali pamoja na kuwaimarisha waamini katika jumuiya hizo.Katika kuziimarisha jumuiya hizo wanawaweka wakfu wazee ambao wataendelea kusimamia kazi ya kitume ambayo wameianzisha.

Swali la kwanza linalotujia katika zama zetu hizi ni lile lisemalo, je sisi tunaweka nguvu zetu katika suala la umoja wa Kanisa letu. Tunaimarishana na kueleweshana mahali ambapo hatuelewi katika imani yetu? Mtume Paulo pamoja na Barnaba wanawaweka wazee wasimamie Jumuiya na wazee hawa walichaguliwa kwa ustadi si kwa mzaha, Je, sisi tuko makini katika kuchagua viongozi wa jumuiya au tunafanya bora liende? Hapana hatupaswi kufanya bora liende bali ni wajibu makini ambao tumekabidhiwa na Mungu mwenyewe tukautende kwa makini.

Mpendwa, hawa viongozi tuliowachagua na kuwasimika tunawajibika kuwaheshimu na kuwasikiliza vema wanatufundisha mambo yahusuyo imani na maadili. Na kwa namna hiyo tutakuwa tunajenga jumuiya yenye nguvu na mshikamano unaolala katika amri mpya na jumuiya mpya inayosimikwa katika Pasaka, ufufuko wa Bwana.

Mpendwa maisha ya ubatizo hayakamiliki mpaka yajikite katika maisha ya Jumuiya yaani kushirikisha vipaji tulivyokabidhiwa wakati wa ubatizo. Kwa kushirikisha vipaji vyetu Jumuiya zetu zitakuwa daima hai badala ya kuwa kusanyiko la matatizo mbalmbali. Katika maisha ya Jumuiya zetu wakati fulani badala ya kuwa chimbuko la furaha linakuwa nni chimbukola matatizo, sasa Je, tukate tamaa? Hapana hatupaswi kamwe, yatupasa kukaza zaidi amri ya mapendo.

Mpendwa, katika somo la pili Mtume Yohane anapoandika kitabu cha Ufunuo anatangaza habari ya furaha na matumaini. Anatupa mwisho wa maisha ya safari ya Mwanadamu, akisema mbingu na nchi mpya vitaumbwa, Mungu atakuwa na watu wake wakimzunguka, atafuta machozi yao, na hakutakuwa na kifo wala maumivu, ni Yerusalemu mpya.

Anawaimarisha wale wanaoteswa kwa sababu ya imani akisema, baada ya Pasaka yote yako chini ya Bwana aliyeshinda mauti. Hata hivyo, kufikia furaha hiyo Kristo Masiha amepitia njia ya msalaba kinyume na wafalme wa dunia ambao hutukuzwa kwa mabavu na kwa damu ya wanyonge.

Msalaba wa Kristo ni kielelezo cha mapendo upeo ya Bwana kwa ulimwengu, ni kielelezo cha ushindi na utukufu wa Kristo dhidi ya dhambi na mauti. Tokea ushindi wa Msalaba Bwana anatangaza utume akisema, ”Pendaneni kama nilivyowapenda mimi”.

Mpendwa msikilizaji, Bwana anapoondoka duniani kurudi kwa Baba yake wa mbinguni, haachi urithi mwingine kama vile mali, nguvu za kutenda miujiza bali anaacha PENDO. Upendo ni zawadi nzuri ambayo kila mmoja akiikamata dunia itabadilika na kuwa mpya, familia itabadilika na kuwa mpya! Bwana anatangaza amri mpya ya Mapendo akitaka kuweka katikati yetu YEYE MWENYEWE ambaye ni chanzo na mwisho wa upendo huo.

Katika Kitabu cha Walawi 19:18 tunapata kusikia, mpende jirani yako kama unavyojipenda wewe mwenyewe, leo Bwana wetu Yesu Kristo anasema pendaneni kama nilivyowapenda mimi. Kristu ni kipimo kipya cha upendo. Katika Walawi, mtu mwenyewe alikuwa kipimo, na Kristu akitambua shida ya mwanadamu wakati fulani hughubikwa na chuki basi anahamisha kitovu cha mapendo.

Jambo la pendaneni kama nilivyowapenda ninyi lazima pia kuliangalia kwa makini. Katika injili ya Luka sura ya 4 anasema, nimekuja kwa ajili ya wanaoteswa, wagonjwa na wale watakaonisulubu, kumbe mwaliko lazima kuweka nguvu katika sura za Kristo ambazo ndo hizo tunazozipata toka Neno lake. Kwa namna hiyo, basi, Mama Kanisa anatualika katika furaha ya Pasaka kuwatazama masikini na wenye shida mbalimbali, na hivi kufanya upendo kuwa ni kitovu cha maisha mapya maisha ya ufufuko. Ndiyo kuyatazama yaliyo ya juu anayotuambia Mtume Paulo tukishafufuliwa na Bwana kwa njia ya ubatizo.

Mpendwa mwana wa Mungu, kama kweli tukipendana Bwana amesema, tutatambulikana kama wanafunzi wake. Hili li wazi sana, ni kama mti unaozaa matunda mazuri watu huendelea kuulina na kutunza na mti huo huendelea kuwa hai. Basi tunarudi tena nyuma tukikumbuka tukishapendana tunaitikia wito wa Bwana yakuwa “mtakuwa mashahidi wangu katika Uyahudi na Samaria yote” Mdo 1:8.

Kwa Hakika mapendo ni alama ya Roho Mtakatifu, kumbe, kama tutakuwa watu wa vurugu na visasi, fujo zinazozuia kazi ya kichungaji hapa hakuna mapendo na hivi hakuna Roho Mtakatifu. Kwa hakika tabia ya Mkristo ni MANTIKI ya UPENDO, kwa njia hiyo anaingia katika njia ya uzima wa milele.

Nikutakie furaha tele katika Dominika hii ya 5 ya Pasaka.

Tumsifu Yesu Kristo.
Tafakari hii imeletwa kwako na Pd. Richard Tiganya C. PP.S.








All the contents on this site are copyrighted ©.