Dr. Olav Fykse Tveit, Katibu mkuu wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni, amehitimisha
ziara ya kichungaji nchini Sudan ya Kusini iliyompatia fursa ya kukutana na kuzungumza
na viongozi wa Makanisa pamoja na viongozi wa Serikali.
Anasema, Makanisa nchini
Sudan Kongwe na Sudan ya Kusini yana fursa ya pekee kabisa katika kuchangia mchakato
wa maendeleo endelevu katika nchi hizi mbili hasa baada ya miaka kadhaa ya vita vya
wenyewe kwa wenyewe sanjari na kuhakikisha kwamba, uhuru wa kidini unaheshimiwa na
kuzingatiwa.
Kuanzia tarehe 23 hadi 25 Aprili 2013, Dr. Tveit alikuwa Sudan
Kongwe na Sudan ya Kusini; nchi mbili zilizojitenga kunako 2011 kama sehemu ya utekelezaji
wa makubaliano ya amani yaliyokuwa yamefikiwa kunako mwaka 2005 baada ya wananchi
wa Sudan ya Kusini kupiga kura ya maoni. Anasema, Makanisa katika nchi hizi mbili
yana dhamana ya kushiriki katika mchakato wa maendeleo kwa kuendelea kushirikiana
na Serikali hasa katika kulinda na kudumisha amani, uhuru wa kuabudu na mshikamano.
Serikali kwa upande wake, inasema, itaendelea kufanya mazungumzo na viongozi
wa Makanisa katika msingi wa kuaminiana ili kwa pamoja waweze kushiriki katika ujenzi
wa Sudan na kwamba, Serikali itaendelea kuhakikisha kwamba, wanapata uhuru wa kuabudu
kadiri ya Katiba ya nchi zao.
Dr. Tveit anasema kwamba, Makanisa yanadhamana
ya kutangaza Injili, jambo ambalo linahitaji umoja na mshikamano wa Makanisa kutoka
Sudan Kongwe na Sudan ya Kusini. Kwa njia hii, wataweza kutolea ushuhuda wa tunu msingi
za maisha ya Kikristo na hivyo kukabiliana na changamoto zinazojitokeza mbele yao
wakati huu wanapojielekeza zaidi katika ujenzi wa nchi baada ya vita vya wenyewe kwa
wenyewe nchini Sudan.