Maadhimisho ya Mwaka wa Imani yaanza kushika kasi mjini Vatican
Baba Mtakatifu Francisko anaanza kushiriki kikamilifu matukio ya Maadhimisho ya Mwaka
wa Imani uliotangazwa na kuzinduliwa na Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na
sita, sanjari na kumbu kumbu ya Jubilee ya miaka 50 ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican
na miaka 20 tangu Mwenyeheri Yohane Paulo wa Pili alipochapisha kwa mara ya kwanza
Katekesimu Mpya ya Kanisa Katoliki, mwongozo makini wa mafundisho tanzu ya Kanisa.
Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi tarehe 27 na Jumapili tarehe 28 Aprili
2013 anatarajiwa kukutana na umati mkubwa wa vijana watakaopokea Sakramenti ya Kipaimara
au ambao tayari wamekwisha pokea Sakramenti hii katika Maadhimisho ya Mwaka wa Imani.
Kilele cha tukio hili la kihistoria katika Maadhimisho ya Mwaka wa Imani ni
hapo Jumapili tarehe 28 Aprili 2013, Jumapili ya tano ya Kipindi cha Pasaka, Baba
Mtakatifu atakapoongoza Ibada ya Misa Takatifu sanjari na kutoa Sakramenti ya Kipaimara
kwa Wakristo 44 wanaopewa dhamana ya kwenda kumshuhudia Kristo kwa maneno na mtendo
yao ya kila siku.
Kundi la Wakristo watakaoimarishwa kwa Sakramenti ya Kipaimara
kutoka sehemu mbali mbali za dunia, wakiwa hapa mjini Vatican watapata Katekesi ya
kina kuhusu imani yao kwa Kristo na Kanisa lake. Wataandamana na hatimaye, kukiri
Imani kwenye Kaburi la Mtakatifu Petro, lililoko kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro
mjini Vatican. Wakristo hawa wanasindikizwa na Mapadre na Makatekista wao waliowaandaa
ili kuweza kushiriki katika Mafumbo ya Kanisa.
Kwa mara ya kwanza Baba Mtakatifu
Francsiko atatoa Sakramenti ya Kipaimara kwa Wakristo 44, kadiri ya taarifa iliyotolewa
na Askofu mkuu Rino Fisichella na viongozi waandamizi kutoka Baraza la Kipapa la Uhamasishaji
wa Uinjilishaji Mpya, walipokuwa wanatangaza matukio makuu ya Maadhimisho ya Mwaka
wa Imani. Wakristo watakaoimarishwa kwa Mapaji ya Roho Mtakatifu ni wale wenye umri
kati ya miaka 11 hadi miaka 55.
Askofu mkuu Rino Fisichella anaendelea kufafanua
kwamba, tarehe 3 hadi 5 Mei 2013, Baba Mtakatifu Francisko katika Maadhimisho ya Mwaka
wa Imani, atakutana na kusali pamoja na vyama vya kitume, ambavyo vimekuwa na Ibada
mbali mbali ndani ya Kanisa. Vyama hivi ni vile vinavyotoka kwenye nchi ambazo zina
utamaduni wa muda mrefu. Wanachama watakuwa na fursa ya kutolea ushuhuda wa imani
yao inayojionesha pia katika sanaa kwa miaka mingi. Itakuwa ni nafasi kwa wanachama
hawa kusali Rozari Takatifu na Baba Mtakatifu Francisko kwenye Kanisa kuu la Bikira
Maria mkuu, tarehe 4 Mei 2013, Saa 12:00 jioni.
Baba Mtakatifu anatarajiwa
kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu na wanachama wa Mashirika haya, Jumapili tarehe
5 Mei 2013, kuanzia saa 4:00 Asubuhi. Haya ni matukio yanayofumbatwa katika hija ya
Maadhimisho ya Mwaka wa Imani. Ni kielelezo cha Mapokeo ya Imani ambayo yamerithishwa
kutoka kizazi kimoja hadi kingine ndani ya Kanisa. Haya ndiyo matukio yanayopaswa
kushuhudiwa katika Imani, Maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa; Kuyamwilisha katika
maisha adili na kuyasali kwa ujasiri, ibada na moyo mkuu.