2013-04-26 08:15:39

Kuna haja kwa Sudan Kongwe na Sudan ya Kusini kuimarisha amani, utulivu na ushirikiano kwa ajili ya maendeleo ya watu wake!


Umoja wa Afrika umezipongeza juhudi zinazoendelea kufanywa kati ya Sudan Kongwe na Sudan ya kusini katika kuimarisha amani na utulivu mpakani mwa nchi hizi mbili pamoja na kuendelea kutatua hatua kwa hatua matatizo yatakayojitokeza tena sanjari na uundwaji wa tume zitakazosimamia utekelezaji wake. Kutokana na umuhimu wake, kuna haja kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, kuchukua hatua madhubuti ili kuhakikisha kwamba, amani na utulivu vinapatikana.

Hayo yamesemwa na Dr. Nkosazana Dlamini Zuma, Kamishina wa Tume ya Umoja wa Afrika alipokuwa anazungumzia mikutano ya dharura iliyokuwa imetishwa na Umoja wa Afrika ili kushughulikia kinzani na migogoro iliyokuwa imejitokeza kati ya Sudan Kongwe na Sudan ya Kusini ili kuimarisha umoja na ushirikiano baina ya nchi hizi pacha, kiasi hata cha kutoa nafasi kwa viongozi wakuu wa nchi kukutana mara kwa mara ili kujadili masuala ya ushirikiano na maendeleo.

Dr. Nkosazana Dlamini Zuma amepongeza pia juhudi za makusudi zinazofanywa na nchi hizi mbili katika kujenga na kuimarisha umoja, amani na maendeleo endelevu ya wananchi wake na kwamba, Umoja wa Afrika utaendelea kusaidia juhudi hizi kwa ajili ya mafao na maendeleo ya wananchi wa Sudan Kongwe na Sudan ya Kusini.







All the contents on this site are copyrighted ©.