2013-04-26 09:19:07

Jicho la haki msingi za binadamu nchini Angola!


Angola ni kati ya nchi ambazo zimepiga hatua kubwa ya maendeleo katika kipindi cha miaka kumi iliyopita hasa baada ya kumalizika kwa vita ya wenyewe kwa wenyewe nchini humo iliyokuwa ni kikwazo kikubwa cha maendeleo.

Ni nchi ambayo imebahatika kuwa na utajiri mkubwa wa madini, kiasi ambacho kimeiwezesha Serikali kuwekeza katika miundo mbinu ya barabara, shule, zahanati, makazi ya watu, nishati na umeme pamoja na kuendelea kuboresha hali ya magereza nchini humo. Licha ya maendeleo makubwa yaliyokwisha kupatikana, lakini kuna ongezeka matabaka ya watu wenye uwezo mkubwa wa kiuchumi na "akina yakhe pangu pakavu tia mchuzi".

Wakati mwingine watu wamelazimishwa kuyahama makazi yao kwa kisingizio cha maendeleo hasa kuzunguka mji mkuu wa Luanda, Angola bila hata ya kushirikishwa katika maamuzi haya. Kuna haja ya kuwa makini na matumizi ya ardhi, wananchi washirikishwe katika maamuzi na utekelezaji wake, pale inapobidi, fidia itolewe kwa wahusika.

Hayo yamesemwa na Bi Navi Pillay Kamishina mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa baada ya ziara yake ya kikazi nchini Angola kwa siku za hivi karibuni. Anasema, amegusia umuhimu wa kuongeza bidii zaidi katika mapambano dhidi ya rushwa na ufusadi; ukosefu wa fursa za ajira kwa kuibua sera na mikakati makini itakayotoa nafasi za ajira hasa miongoni mwa vijana, ili kuleta uwiano mzuri zaidi wa hali ya maisha nchini Angola, vinginevyo, watu watakata tamaa na matokeo yake ni uvunjifu wa misingi ya haki, amani na utulivu kama inavyojionesha katika baadhi ya nchi Barani Afrika.

Maendeleo ya miundo mbinu hayana budi kwenda sanjari na haki msingi za binadamu ili kuimarisha mafao na maendeleo yaliyokwisha kupatikana baada ya wananchi wa Angola kujifunga kibwebwe! Uandikishaji wa uzazi na vifo ni jambo muhimu sana katika kupanga mikakati ya maendeleo kwa sasa na kwa siku za usoni.

Jambo hili linapaswa kufanyiwa kazi na Serikali hata kama kwa sasa si kati ya vipaumbele vya Serikali ya Angola ambayo kwa sasa inasema, inapenda kujielekeza zaidi katika kuziwezesha familia pamoja na kuboresha hali ya maisha ya wananchi wa Angola. Serikali imeongeza bajeti ya shughuli za kijamii kwa mwaka 2013.

Katiba Mpya ya Angola pamoja na kuundwa kwa Mahakama ya Katiba ni kati ya mafanikio makubwa nchini Angola katika mchakato wa kusimama kidete kulinda na kutetea haki msingi za binadamu. Haki za wanawake na ushiriki wao katika vikao vya maamuzi na utekelezaji zimeongezeka kwa asilimia 34%. Miaka miwili iliyopita, Bunge la Angola lilitunga na kupitisha sheria dhidi ya vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia.

Sheria hii inaendelea kuimarishwa kwa kutoa elimu kwa umma ili kuwathamini na kuwajali wanawake. Maboresho ya sheria hayana budi kwenda sanjari na uwezekano wa raia kupata haki zao msingi bila "kigugumizi" chochote. Hii inatokana na ukweli kwamba, wakati mwingine, vikosi vya ulinzi na usalama vimetumia nguvu kubwa kuzima maandamano ya amani kwa kisingizio cha usalama wa taifa.

Kuna viongozi wawili walitekwa nyara Mei, 2012 hadi leo hii anasema Bi Navi Pillay hawajulikani waliko, ingawa Serikali inasema inaendelea kufanya uchunguzi. Viongozi wanaotumia vibaya madaraka yao wanapaswa kuwajibishwa kwa kufikishwa mbele ya sheria ili haki iweze kutendeka. Kuna uhuru mkubwa wa vyombo vya habari, lakini baadhi ya waandishi wa habari wanaoshughulikia na masuala ya uchunguzi, wakati mwingine wanashindwa kutekeleza wajibu wao kutokana na hofu ya sheria kandamizi.

Uhuru wa vyombo vya habari ni sehemu ya mchakato wa kuimarisha demokrasi, utawala wa sheria, ukweli na uwazi. Hapa kuna haja ya kuendelea kuboresha sheria kuhusu: uhuru wa kukutanika, kugoma na kuchunguza ili ukweli uweze kufahamika kwani watu wana haki ya kuhabarishwa kile kinachoendelea ndani ya Jamii zao! Ili kuepusha migogoro, kinzani na malumbano yasiyokuwa na tija wala maendeleo kwa wanachi, kuna haja kwa Serikali kujenga na kuimarisha majadiliano na vyama vya kiraia.

Serikali ya Angola ilifuta adhabu ya kifo yapata miaka 20 iliyopita na kwamba, imeendelea kuridhia Itifaki mbali mbali za kimataifa kuhusiana na haki msingi za binadamu, ingawa bado haijaridhia itifaki inayopiga rufuku mateso na ubaguzi wa rangi, ingawa kwa nchi ya Angola haya si matatizo makubwa.

Bi Navi Pillay, Kamishina mkuu wa haki za binadamu kutoka Umoja wa Mataifa anaendelea kusema kwamba, makazi duni nchini Angola ni matokeo ya vita ya wenyewe kwa wenyewe nchini humo, kiasi cha kuwafanya watu wengi licha ya maendeleo yaliyopatikana katika miaka ya hivi karibuni, kuendelea bado kuogelea katika dimbwi la umaskini wa hali na kipato.

Sera na mikakati ya uzalishaji wa fursa za ajira ni mambo ambayo yanapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza kama sehemu ya mchakato wa maboresho ya hali ya wananchi wa Angola, ili hatimaye, wao pia waweze kuishi mahali bora zaidi na utu wao kuheshimiwa na kuthaminiwa.

Wageni na wahamiaji wanaotafuta fursa za ajira na hali nzuri ya maisha wanapaswa kuheshimiwa pia kwani wao pia wanachangia katika uchumi na maendeleo ya Angola. Haki za wageni na wahamiaji zinapaswa kuheshimiwa mintarafu sheria na mikataba ya kimataifa. Hili ni tatizo tete kwani kuna wahamiaji na wakimbizi wengi kutoka DRC wanaoingia nchini Angola ili kutafuta hifadhi ya maisha. Jambo hili linahitaji kushughulikiwa kwa karibu zaidi na wakuu wa Nchi za Kusini mwa Afrika ili kuona ni jinsi gani wanavyoweza kulipatia tatizo hili ufumbuzi wa kudumu. Takwimu zinaonesha kwamba, asilimia 80% ya wakimbizi wote walioko nchini Angola ni wale wanaotoka DRC.

Tatizo la wakimbizi na wahamiaji haramu limepelekea pia kuibuka kwa vitendo vya ubakaji na udhalilishaji wa kijinsia, hasa kwa wanawake na wasichana, vitendo vinavyofanywa wakati mwingine na Wanajeshi na Polisi waliopewa dhamana ya kulinda usalama wa raia. Bi Navi Pillay anasema kuna haja ya kufanya uchunguzi wa kina ili kubainisha ukweli wa mambo haya na wahusika wakikamatwa wafikishwe kwenye mkondo wa sheria. Hili ni tatizo ambalo limekuwepo nchini Angola kwa takribani miaka kumi sasa.

Serikali ya Angola inapaswa kuboresha mikakati na sera zake juu ya haki msingi za binadamu kwa kuridhia mkataba wa Kanuni za Paris, linayozitaka nchi wanachama kuanzisha taasisi ya kitaifa itakayoshughulikia haki msingi za binadamu, miswada ya sheria pamoja na ushirikiano wa karibu zaidi na vyama vya kiraia ambavyo vina mchango mkubwa katika maendeleo ya watu. Serikali ya Angola imesema, italifanyia kazi wazo hili kwa kushirikiana na Kamishina wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa.

Bi Navi Pillay, Kamishina mkuu wa haki za binadamu kutoka Umoja wa Mataifa anasema, kwa hakika ziara yake ya kikazi nchini Angola imekuwa na manufaa makubwa kama sehemu ya mchakato wa kutambua, kuimarisha, kulinda na kudumisha haki msingi za binadamu.

Hizi ni haki zinazotekelezwa kwa kuzingatia Katiba ya nchi ambayo ndiyo sheria mama; Mahakama pamoja na taasisi ambazo kwa namna moja au nyingine zinajihusisha na masuala ya haki mzingi za binadamu. Angola ikiendelea katika maboresho haya inaweza kuwa ni mfano wa kuigwa kwa nchi za Kiafrika na duniani kwa ujumla.









All the contents on this site are copyrighted ©.