Katika mazingira ya Mwaka wa Imani, Jumatano , Askofu Mkuu Rino Fischella, Rais wa
Baraza la Kipapa kwa ajili ya ukuzaji wa Uinjilishaji Mpya, aliwasilisha matukio mawili,
kwanza ni mkutano wa muda wa siku mbili 27 -28 Aprili juu ya Sakramenti ya Kipaimara,
na tukio la pili Siku ya udugu na matendo ya Huruma, hapo tarehe 3-4 Mei.
Katika
mahojiano na Fausta Speranza wa Radio Vatican , Askofu Mkuu Rino Fischella, amethibitisha
kwamba, Papa Francisko, ameridhia matukio yote yaliyopitishwa na Papa Benedikto
XVI, katika wazo lake la kuwa na Mwaka wa Majitolea na Imani. Hivyo tukio lijalo
ni kwa ajili ya wale watakaopata daraja la Kipaimara kwa mwaka huu wa 2013. Tayari
idadi ya watakao pokea Sakramenti ya Kipaimara inatajwa kuwa elfu sabaini (70,000)
lakini kuna mwelekeo wa idadi hiyo kuongezeka.
Na kwamba Papa Francisko atatoa
Sakramenti ya Kipaimara kwa wafuasi wa Kristu, wapatao 44 watakao toka Bara mbalimbali
za dunia, wengi wao wakiwa vijana. Pia katika kundi la watu wazima, mmoja wao ni
kutoka Cape Verde, mwenye umri wa miaka 55. Na wengine watatoka katika makundi mbalimbali
ya kijamii akiwemo kijana mlemavu, mwingine atatoka katika eneo lililokumbwa na
tetemeko la aridhi lakini wote katika ujumla wao, wanakuwa ni ushuhuda halisi wa
umoja wa Kanisa la ulimwengu.