2013-04-25 07:35:39

Jengeni urafiki na Yesu kwa Njia ya: Sala, Neno la Mungu na Maisha ya Kisakramenti


“Siwaiti tena watumishi bali nawaita rafiki, kwa kuwa yote niliyoyasikia kwa Baba yangu nimewaarifu”. Haya ni maneno ya Kristu kwa wafuasi wake, lakini maneno haya yanalia leo masikioni mwako kijana na yana uzito na umuhimu ule ule. Wewe ni rafiki wa Kristo, ndivyo anavyokutambua. Kazi kwako kujiuliza je, wewe ni mwaminfu kiasi gani katika urafiki huo. RealAudioMP3
Labda kabla ya kufika katika swali hilo, jiulize kwanza kama wewe mwenyewe unajitambua hivyo na kumkubali. Karibu sana ndugu msikilizaji katika hema letu vijana leo. Chukua nafasi yako na kwa furaha kabisa na uelewa wa kirafiki tutafakari pamoja juu ya urafiki wetu na Kristo.
Tuanze kwa kuona tabia na kisha umuhimu wa rafiki katika maisha. Rafiki ni mtu aliye karibu nawe. Ukaribu huu sio ukaribu wa ujirani, bali ni ukaribu wa mahusiano. Kumbe yawezekana kabisa ukawa mbali sana na mtu huyo lakini yeye bado ni rafiki yako kipenzi. Kumbe, umbali hauvunji urafiki. Urafiki unakuwepo na udumu kwa ule ukaribu wa ndani uliopo kati yako na rafiki yako. Rafiki hatambuliki kwa ukaribu wa kijirani bali rafiki wa kweli hujulikana wakati wa shida.
Rafiki ni mtu mwenye kukupenda. Upendo ni hisia za ndani ambazo hazipimiki kwa urahisi. Ni wazi kwamba unaweza kutambua upendo wa mtu kwa namna anavyokusalimu, kwa namna anavyokuchukulia, kwa namna anavyokutendea. Kumbe kuna ishara za nje zinazoweza kuashiria upendo wa mtu. Hata hivyo, napenda uchukue tahadhari katika hili. Wengi wanaweza kuonesha ishara za nje za wazi kana kwamba wanakupenda lakini ndani mwao wana masilahi binafsi. Watu wa namna hii wakishapata wanachohitaji au kufikia malengo yao hutaona tena upendo wao.
Kumbe, zingatia zaidi hisia za ndani zaidi na ishara nyingi za kudumu zinazoendana na upendo huo. Tambua pia kuwa rafiki hujitahidi kuishi kadiri ya hali halisi. Mkiishi vitu vya kujilazimisha sana eti kuoneshana upendo inabidi muwekane sawa juu ya uhalisia wa urafiki wenu.
Rafiki ni mkweli na muwazi kwako. Kawaida marafiki huongea mara kwa mara na kuelezana ukweli. Ukweli na uwazi ni kujifunua kwa mwenzio, kujitambulisha wazi jinsi ulivyo bila kufichaficha. Mahusiano ya kweli, si ya ulaghai na unafiki. Katika hali hiyo marafiki hukosoana na kurekebishana kwa upendo. Urafiki wa kweli hauendekezi ushindani usio na msingi.
Kudumu katika mahusiano ya karibu ni sehemu ya tabia ya urafiki. Inawezekana mkawa mbali lakini mnawasiliana mara kwa mara. Hapa uwe makini kidogo. Ile mara kwa mara inategemea na njia za mawasiliano, muda wa kila mmoja, hali zenu kiuchumi, kijamii, kisiasa na kadhalika. Yote haya huathiri mawasiliano. Pamoja na hayo, jiulize je, unaweka kipaumbele kiasi gani katika kuwasiliana na rafiki yako?
Uwepo kifizikia pia ni muhimu katika urafiki. Hata pamoja na umbali. Basi, yafaa kutafuta nafasi kadha wa kadha ili kuonana. Uwepo wa rafiki si lazima kuwa na maongezi marefu na porojo zisizo na mipaka. Mnaweza kukutana na kuwa pamoja, kwa maongezi machache. Mara nyingine unaweza ukawa unahitaji tu uwepo wa rafiki bila kusema neno. Kuonana katika hali ya ukimya na utulivu lakini ukafaidika na faraja kutoka kwa rafiki yako.
Duh!, Ee Bwana weee! Unaelewa kadiri ninavyoongea kuhusu urafiki naona ninachana tu mistari na dakika zinayoyoma. Sasa ni vizuri tuwakane sawa mapema. Hayo tuliyojadiri kuhsu urafiki, kwa kweli ndivyo Kristo anakuhitaji wewe kijana uwe kwake. Yeye anakupenda na kukuamini, anapenda wewe pia umpende na kumwamini.
Kashuka na kuishi katika hali ya kibinadamu ili awe karibu nawe, naye amebaki nawe katika s
Sakramenti mbali mbali na hasa katika Ekaristi Takatifu. Kristo anapenda kuonana nawe katika Sakramenti hizo. Kutana na rafiki yako katika Ubatizo, Kitubio, ndoa na kadhalika. Jiweke katika hali nzuri kupokea Ekaristi Takatifu uishi na kudumu naye. Chukua muda kila unapoweza, walau mara moja kwa juma, ukae mbele ya Yesu wa Ekaristi katika utulivu na kumwabudu.
Mweleze Kristu shida zako, kuwa wazi kwake. Sali kwa bidii, ongea naye katika Neno lake, soma Injili Takatifu, Itafakari na Kuimwilishwa katika maisha. Usimwogope rafiki yako, huna sababu ya kumwogopa bali yafaa umpende na kumkaribia. Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, mwaka 2005 alikwambia “usimwogope Kristo, maana yeye hachukui chochote kutoka kwako, badala yake ukimpokea na kudumu naye anakupa kila kitu”
Tuonane tena juma lijalo. Kutoka Studio za Radio Vatican, ni sauti ya kinabii, Padre Celestine Nyanda.








All the contents on this site are copyrighted ©.