Ekaristi Takatifu ni kiini cha maisha na utume wa Kanisa
Baraza la Maaskofu Katoliki Costa Rica hivi karibuni limeadhimisha Kongamano la Nne
la Ekaristi Takatifu Kitaifa, lililoongozwa na kauli mbiu ""Ekaristi Takatifu. Mkate
wa maisha ya watu wetu". Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe ulioandikwa kwa niaba
yake na Kardinali Tarcisio Bertone, Katibu mkuu wa Vatican, aliwatakia kheri na baraka
washiriki wote wa kongamano kwa kutambua kwamba, Maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi
Takatifu ni kiini cha maisha na utume wa Jumuiya ya Wakristo.
Baba Mtakatifu
kwa namna ya pekee aliwaalika wajumbe kufanya tafakari ya kina na kusali zaidi, kwani
Ekaristi Takatifu ni kiini cha maisha ya Kanisa; mahali ambapo waamini wanatolea sadaka
ya shukrani na sifa, tayari kujitosa kimasomaso kwa ajili ya kushiriki katika mchakato
wa Unjilishaji mpya, dhamana inayovaliwa njuga na Mama Kanisa katika Mapambazuko ya
Millenia ya Tatu ya Ukristo.
Maadhimisho ya Ekaristi Takatifu yajenge na kuimarisha
umoja miongoni mwa waamini; wajitahidi kujichotea neema na baraka kutoka mbinguni
ili kushiriki katika ujenzi wa dunia inayosimikwa katika misingi ya haki, amani, upendo,
mshikamano na upatanisho mintarafu ujumbe kutoka kwa Kristo mwenyewe.
Baba
Mtakatifu Francisko amewaweka waamini wote nchini Costa Rica chini ya ulinzi na usimamizi
wa Bikira Maria na Malaika, wanapoendelea na hija ya maisha yao kuelekea mbinguni
kwa Baba. Baba Mtakatifu amewapatia wote baraka zake za kitume. Ujumbe wa Baba Mtakatifu
katika Maadhimisho haya ulisomwa kwa niaba yake na Askofu mkuu Piero Marini, Rais
wa Tume ya Kipapa ya Makongamano ya Ekaristi Takatifu Kimataifa.