Vitumieni Vipaji vyenu kwa manufaa ya wote - Papa ahimiza Vijana
Baba Mtakatifu Francisko, mapema Jumatano , baada ya kuzungukia maelfu ya mahujaji
a wageni waliokusanyika katika uwanja wa Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro la Vatican,
akiwa katika gari dogo la wazi, alitoa Katekesi kama kawaida ya kila Jumatano. Mafundisho
ya Papa yameendelea kuzungumzia imani, leo yakilenga ujio wa pili wa Kristu "Yeye
atakuja tena kwa utukufu, kuwahukumu walio hai na wafu". Papa amesema, kama ilivyo
historia ya binadamu, iliyoanza na kuumbwa kwa mwanaume na mwanamke kwa mfano wa Mungu,historia
hiyo inatatimizwa na ujio wa Pili wa Kristu na hukumu yake ya mwisho. Papa amekumbusha
, kwa mara nyingi binadamu husahau misingi miwili ya historia hii na zaidi imani
juu ya ujio wa pili wa Kristu na hukumu ya mwisho, ambavyo mara nyingi, vimeonekana
kutoeleweka wazi kwa waamini. Yesu katika maisha yake hapa duniani, alilfundisha
kwa kutoa mifano mingi, juu ya ujio wake wa mwisho. Papa aliendelea kurejea
maandiko mengi ya Injili, yanayosaidia kumzamisha mtu katika uelewa wa fumbo hili.
Alitaja, mfano wa wanawali kumi , watano wenye busara na watano wapumbavu, na pia
mfano wa hukumu ya mwisho , kama ilivyoelezwa katika Injili ya Mtakatifu Matayo( 24:29-31)
(25: 113). Anasema mifano hiyo inatukumbusha sisi kwamba ni lazima kiroho kuwa
tayari kukutana na Bwana atakapokuja. Na mfano wa talanta, husisitiza wajibu wetu
wa kutumia vipaji tulivyojaliwa kama zawadi kutoka kwa Mungu, kwa ajili ya kufanikisha
faida kwa wengine wengi. Amehoji ni kwa jinsi gani, tumevitumia vipaji hivyo tulijaliwa
bure na Mungu. Na kama ni haki kwa Mkristu , kufungua ndani ya moyo wake, neema na
manufaa na mazuri yote ya kuishi na Kristu, bila ya kuwatangazia wengine. Kwa
ajili hiyo, Papa aliwageukia vijana waliokuwa miongoni mwa mahujaji na wageni , akisema,
“ ninyi vijana wengi mliokusanyika hapa, mkiwa mmeianza tu hija ya maisha, je mmewahi
kufikiria kwa jinsi gani, mnaweza kuvitumia vipaji mlivyojaliwa na Mungu, kwa ajili
ya faida ya wengine, ndani ya kanisa na dunia yetu kwa ujumla. Amewasisitizia
wasifiche vipaji vyao, bali wajitokeze kwa ushupavu mkuu na waipanue mioyo yao,
katika kuwahudumia wengine. Amesema, "Maisha mliyopewa si kwa ajili ya kuyafungia
kwa uchoyo na ubinafsi lakini mmeyapewa kwa ajili ya kuhudumia wengine, na hasa wahitaji
kama wazee na wagonjwa. Baada ya Katekesi, Papa alisalimia na kutoa Baraka kwa
makundi mabalimbali, wazee, wanadoa wapya na wagonjwa.