2013-04-24 07:49:35

Mikakati ya SAUT katika maboresho ya elimu nchini Tanzania


Kanisa Katoliki nchini Tanzania ni kati ya wadau wakuu wa sekta ya elimu. Kanisa limekuwa likichangia kwa namna ya pekee katika maboresho ya elimu yanayolenga kuwajengea wanafunzi uwezo wa kupambana na mazingira yao, ili dunia iweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi. RealAudioMP3

Familia zenye uwezo wa chini zimekuwa zikipewa kipaumbele cha pekee katika mikakati ya elimu inayotolewa na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania.

Katika mahojiano na Radio Vatican, Mheshimiwa Padre Charles Kitima, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augostino cha Tanzania, SAUT anapembua baadhi ya mikakati inayotekelezwa na SAUT katika maboresho ya elimu ya juu nchini Tanzania. Anasema, mkakati wa kwanza unapania kuwaandaa wahadhiri wenye upeo, moyo na ari ya kuweza kuwahudumia watanzania mintarafu sera na malengo ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania.

Hadi sasa SAUT ina wahadhiri wapatao 1,000 wanaotekeleza majukumu yao kwenye Matawi 11 ya SAUT yaliyoenea sehemu mbali mbali za Tanzania. SAUT inapenda kuona kwamba, wahadhiri wote wanaofundisha SAUT wanafikia kiwango cha shahada ya uzamivu.

Hii ndiyo maana SAUT inaendelea kuwekeza sana katika mkakati huu ili kuboresha kiwango cha elimu nchini Tanzania na wale wanaopikwa hapo wawe wameiva barabara tayari kujimwaga uwanjani kuwahudumia watanzania.

Kwa miaka kumi hivi, SAUT imeendelea kuwa na kiwango cha chini ya ada ikilinganishwa na Vyuo vingine nchini Tanzania. Lengo ni kuwajengea watanzania utamaduni wa kulipa, kwa kujinyima na kwa njia ya sadaka, ili kuwapatia watoto wao fursa ya elimu ya juu kwani elimu ni mkombozi. Kutokana na sera hii, SAUT imeendelea kuwa na idadi kubwa ya wanafunzi wanaojiunga na Chuo Kikuu hiki.

Kuna jumla ya wanafunzi 28,000 kutoka SAUT na CUHAS, yaani Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Afya ba Sayansi Mwambata Bugando. Padre Charles Kitima anasema kwamba, Kanisa Katoliki Tanzania linahudumia wanafunzi wote hawa katika Vyuo vyake vikuu na huu ni mchango mkubwa kwa Jamii ya Watanzania na kwamba ada wanayotoza inalipika.

SAUT imeamua kutumia vigezo vya juu wakati wa kudahili wanafunzi wanaotaka kujiunga na SAUT, lengo ni kuwa na kiwango cha juu cha elimu ili wanafunzi wanaotoka SAUT wawe na viwango stahiki tayari kukabiliana na soko la ajira ndani na nje ya nchi.









All the contents on this site are copyrighted ©.