Maadili, haki msingi za binadamu na uwiano wa maendeleo endelevu!
Mafundisho Jamii ya Kanisa Katoliki ni nyenzo muhimu sana katika Uinjilishaji kwani
inapania kwa namna ya pekee kuyatakatifuza malimwengu kwa kuweka mahusiano ya kibinadamu
na ya jamii katika mwanga wa Injili. Kanuni za Mafundisho Jamii ya Kanisa zinatokana
na sheria asili zinazoimarishwa na kukomazwa katika imani ya Kanisa kwa njia ya Injili
ya Kristo inayoshuhudiwa katika matendo.
Kanisa ni mahiri sana katika kuyashughulikia
masuala yanayohusu binadamu na linaendelea kuchanja mbuga kuelekea kwenye "mbingu
mpya na nchi mpya". Kwa mujibu wa imani na kwa kujihusisha katika maisha halisi ya
binadamu, jambo ambalo Kanisa linataka liwe wazi kwa kila mtu ili kusaidia mchakato
wa watu kuishi kwa kuzingatia upeo wa maana halisi wa maisha. Binadamu anayeishi mintarafu
hadhi ya utu wake anatoa utukufu kwa Mungu aliyewakirimia watu wote hadhi ya utu wa
binadamu kwani wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.
Ni kutokana na uelewa
huu mpana Baraza la Maaskofu Katoliki Burkina Faso kwa kipindi cha miaka mitano sasa
limekuwa likiandaa Juma la Tafakari ya Maisha Jamii linalosimamiwa na kuratibiwa na
Tume ya Haki na Amani ya Baraza la Maaskofu Katoliki Burkina Faso. "Maadili, haki
msingi za binadamu na maendeleo endelevu ya wananchi wa Burkina Faso: uwiano na matarajio
katika mwanga wa Mafundisho Jamii ya Kanisa" ndiyo kauli mbiu iliyoongoza maadhimisho
haya kwa mwaka 2013. Lengo la Maadhimisho ya Juma la Tafakari ya Maisha Jamii
wanasema Maaskofu ni kuliwezesha Kanisa kutekeleza wajibu na dhamana yake katika maendeleo
ya wananchi wa Burkina Faso mintarafu haki msingi za binadamu, utu na heshima ya binadamu
aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Serikali ya Burkina Faso imelishukuru na kulipongeza
Kanisa kwa ushiriki wake katika kusimama kidete kulinda na kutetea utu na heshima
ya binadamu pamoja na kuwajengea uwezo wananchi ili kupambana kikamilifu na hali yao
ya maisha.
Tume ya haki na amani ya Baraza la Maaskofu Katoliki Burkina Faso
inasema, hizi ni fursa zinazopania kutoa majiundo endelevu kwa waamini ili waweze
kukua na kukomaa katika imani, matumaini na mapendo. Lengo ni kuwajengea uwezo waamini
na watu wenye mapenzi mema ili waweze kuwa ni chumvi na mwanga wa dunia unaopania
kwa namna ya pekee kushiriki kikamilifu katika mchakato wa waamini walei kuyatakatifuza
malimwengu.
Tafakari hizi zimewawezesha pia waamini kutambua na kushiriki
katika mikakati ya Kanisa dhidi ya rushwa na ufisadi; umaskini na umuhimu wa waamini
wa Kanisa Katoliki kushiriki kikamilifu katika maisha ya kijamii, kisiasa na kiuchumi,
ili kuchangia kwa hali na mali, lakini zaidi kwa njia ya ushuhuda wa maisha yao amini,
yanayoonesha imani katika matendo.
Itakumbukwa kwamba, kanuni msingi za Mafundisho
Jamii ya Kanisa zinakazia kwa namna ya pekee: mshikamano unaoongozwa na kanuni ya
auni; mafao ya wengi; upendeleo wa pekee kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni
mwa Jamii; matumizi sahihi ya rasilimali kwa ajili ya wengi; haki na amani.