Shirika la Kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa, UNICEF, tarehe 24 Aprili 2013 linaanza
Kampeni ya chanjo kwa kipindi cha juma zima ili kupunguza vifo vya watoto wadogo vinavyoendelea
kutokea sehemu mbali mbali za za dunia, lakini kwa namna ya pekee Barani Afrika na
nchi nyingine zinazoendelea duniani. Lengo ni kuokoa maisha ya watoto kati ya millioni
mbili hadi tatu kila mwaka. Hii ni changamoto kubwa kwa Jumuiya ya Kimataifa.
Katika
kipindi cha mwaka 2011, jumla ya watoto millioni 22.4 walipatiwa chanjo, ikiwa ni
ongezeko la watoto millioni moja, ikilinganishwa na watoto waliochanjwa katika kipindi
cha mwaka 2010. UNICEF inasema, mikakati yake inakwamishwa na baadhi ya nchi wanachama
ambazo zimeshindwa kuchangia ili kufanikisha kampeni hii.
Kati ya nchi 193
wanachama wa UNICEF ni nchi 152 ambazo zimechangia hadi sasa. Watoto wanaotoka kwenye
familia maskini ndio wanaopoteza maisha kwa kukosa huduma za chanjo, ikilinganishwa
na familia zenye uwezo mkubwa kiuchumi au zile zinazoishi vijijini.
Serikali
husika zinapaswa kuwa na sera na mikakati madhubuti ili kwamba, chanjo iweze kutolewa
kwa wote bila ubaguzi. Kampeni hii inawashirikisha pia watu wenye mapenzi mema ambao
wanaweza pia kuchangia ili kuokoa maisha ya watoto wengi sehemu mbali mbali za dunia.