IMF na WB watangaza vita dhidi ya baa la umaskini hadi kufikia mwaka 2030!
Shirika la Fedha Kimataifa na Benki ya Dunia kwa pamoja, wameamua kulivalia njuga
baa la umaskini wa kipato duniani ili ifikapo mwaka 2030 liwe limepunguzwa walau kwa
asilimia 3% ya idadi ya watu duniani.
Hii ni sawa na watu billioni mbili.
Hayo yamo kwenye taarifa ya pamoja iliyotiwa mkwaju na Mashirika haya fedha kimataifa
katika mkutano wa wanachama uliojadili kuhusu maendeleo endelevu kwa kuzijumuisha
nchi wanacahama 25.
Wadau wa maendeleo wanabainisha kwamba, mkakati huu unapania
kuweka historia kwa Jumuiya ya Kimataifa katika mapambano dhidi ya baa la umaskini
duniani. Hadi sasa kuna jumla ya watu billioni moja, laki mbili na hamsini ambao bado
wanaogelea kwenye umaskini wa kutupwa, kadiri ya takwimu za Benki ya Dunia zilizotolewa
kunako mwaka 2010.
Lakini wachunguzi wa masuala ya maendeleo wanasema, pengine
takwimu hizi hazioneshi hali halisi ilivyo kwani kumekuwepo na maendeleo makubwa katika
harakati za utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo ya Millenia ifikapo mwaka 2015. Itakumbukwa
kwamba, kwenye miaka ya 1990 baa la umaskini lilikuwa linawaandama asilimia 43% ya
idadi ya watu duniani.
Viongozi wakuu wa Mashirika ya Fedha Duniani wanaonesha
matumaini ya kuweza kufanikiwa kupunguza baa la umaskini ifikapo mwaka 2030. Ili kufanikisha
mikakati hii kuna haja kwa Serikali mbali mbali kuwa sera makini zinazozalisha na
kulinda fursa za ajira kwa wananchi wake.
Idadi ya watu wasiokuwa na fursa
za ajira duniani kwa sasa imefikia watu millioni 198, kati yao kuna vijana millioni
74; hali ambayo Shirika la Kazi Duniani linasema kwamba, kwa hakika idadi hii inatisha.