2013-04-22 10:06:25

Mshikamano wa kidugu na waathirika wa vita Mashariki mwa DRC


Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Congo imetoa dhamana kwa Shirika la Misaada la Kanisa Katoliki Caritas DRC kusimamia na kugawa msaada wa mshikamano wa kitaifa kwa watu walioathirika na vita Mashariki mwa DRC. Kampeni hii ya mshikamano wa kidugu kitaifa inatarajiwa kudumu walau kwa muda wa miezi mitatu na imezinduliwa hivi karibuni na Bwana Charles Naweji, Waziri wa Jamii, misaada na mshikamano wa kitaifa.

Hii inatokana na ombi lililotolewa na wadau mbali mbali wa misaada ya kijamii kutoka ndani na nje ya DRC kutaka dhamana ya kusimamia na kugawa misaada ya mshikamano wa kitaifa wapewe Caritas DRC. Wananchi na watu wenye mapenzi mema ndani na nje ya DRC kwa namna ya pekee wanaalikwa kuonesha mshikamano wa kidugu na wananchi wa DRC wanaoishi Mashariki, ambayo kwa takribani miaka ishirini wameendelea kuathirika kutokana na vita inayorindima sehemu hizo.

Shirika la Habari za Kimissionari FIDES linabainisha kwamba, kampeni ya mshikamano wa kitaifa inaendeshwa na Mashirika ya Kitawa, Mashirika Yasiokuwa ya Kiserikali na Watu binafsi ambao watapita sehemu mbali mbali za DRC kuomba na kukusanya misaada kwa ajili ya waathirika wa vita Mashariki mwa DRC.








All the contents on this site are copyrighted ©.