Changamoto zinazoikabili Jumuiya ya Kimataifa kuhusiana na uhuru wa kuabudu
Uhuru wa kuabudu katika ulimwengu mamboleo ni mada iliyochambuliwa na washiriki wa
kongamano la kimataifa kuhusu uhuru wa kidini lililofanyika mjini Vatican kwa kuandaliwa
na Wanamtandao wa ”Technology, Entertainment, Design”, TED chini ya udhamini wa Baraza
la Kipapa la Utamaduni.
Kongamano
hili limehudhuriwa na watu kutoka medani mbali mbali za maisha, taaluma na imani.
Kardinali Gianfranco Ravasi, Rais wa Baraza la Kipapa la Utamaduni katika
mada yake amesisitiza swala la jamii ya binadamu kujifunza kuishi pamoja kama ndugu
na kinyume chake ni maangamizi ya pamoja. Maneno haya yanaonesha umuhimu wake hasa
katika nyakati hizi. Anasema kwamba, uhuru wa kuabudu si jambo la hiari bali ni jambo
la lazima na ni kati ya haki msingi za binadamu.
Katika ulimwengu wa utandawazi
na maendeleo ya sayansi na teknolojia, utamaduni wa kuishi pamoja na watu wenye imani
tofauti ndilo jibu la msingi katika zama hizi za mwingiliano wa watu wanaotoka nchi
mbali mbali kila mtu akiwa na mila na desturi zake.
Kanisa Katoliki linaamini
misingi ya uhuru wa kuabudu na haliwezi kufanya tofauti na hivyo kwa kuwa hali hiyo
ndiyo inayoleta amani katika jamii. Uhuru wa kuabudu ni kiini cha mafundisho yake
katika jamii kama linavyofundisha kwenye hati inayo husu hadhi ya mwadamu (Dignitate
Humanae) inayosisitiza uhuru wa mtu kuabudu, na kwamba jambo hili halipaswi kuchanganywa
na mmabo ya siasa kwa kuzingatia ukweli unaotokana na Mafundisho ya Yesu mwenyewe
kwamba ni vyema kumpa Kaisari kilicho cha Kaisari na kumpa Mungu kilicho cha Mungu
bila kuchanganya.
Mambo haya yanapotenganishwa hayamaanishi kwamba mwanadamu
amegawanyika, bali yanaonesha hali ya kuziheshimu amari za kidunia na papo hapo kutoa
kipaumbele kwa mambo yanayohusu dhamiri ya mtu mwenyewe. Katika mada yake ameendelea
kusisitiza swala la uhuru wa mikusanyiko kwa ajili ya mambo ya ibada ambayo yanahusisha
kufundisha, kuhubiri, kushuhudia pamoja na kushiriki katika mchakato wa Uinjilishaji
mpya.
Kardinali Ravasi anasema kwamba, bado kuna nchi nyingi duniani ambako
serikali zinazuia uhuru wa mtu kuabudu jambo ambalo ni kinyume si tu cha haki msingi
za binadamu bali pia ni kukosa kuheshimu uhuru na hadhi aliyo nayo kila mwadamu aliyeumbwa
kwa sura na mfano wa Mungu; na nchi zingine zinabagua dini za wananchi wao na kuwawekea
vikwazo vya makusudi ili wasiweze kuabudu. Sehemu mbalimbali za dunia kuna baadhi
ya serikali zinajichukulia madaraka ya kuzuia mikusanyiko ya ibada na badala yake
wanazipatia kipaumbele shughuli zingine za kijamii.
Baadhi ya Serikali zinajiingiza
hata kwenye maswala ya maisha ya kila siku ya wananchi wao na mara pengine ni Serikali
inaamua kuruhusu au kutoruhusu shughuli za kiibada kufanyika. Kuna watu wanatishiwa
maisha kwa ajili ya imani yao, hasa wale ambao idadi yao ni ndogo zaidi. Kuna baadhi
ya nchi ambako baadhi ya watu hawaruhusiwi kufanya sala binafsi wala kufundisha dini
ya Kikristo, wafanyakazi wanalazimishwa kufuata mitazamo kinyume kabisa na dhamiri
zao na hata wakati mwingine wanalazimishwa kukumbatia utamaduni wa kifo kwa vuitisho
vya kufukuzwa kazi. Dhamana ya dini katika jamii yoyote ile ni kujenga jamii inayoishi
kwa mshikamano na pendo na si kujenga chuki na misigano ya maisha.
Rabbi
mkuu David Rosen wa Jumuiya wa Kiyahudi nchini Ireland, akitoa mchango wake katika
Kongamano hilo ameelezea kwamba, kuna haja ya waamini wa dini mbali mbali kukuza mahusiano
ya karibu katika kufahamiana; kuzifahamu imani za wengine na kuziheshimu.
Watu
wa imani mbalimbali wataweza kufanya kazi kwa pamoja ikiwa wataweza kuondoa hisia
hasi ambazo mara nyingi zinajengeka kwenye jamii kuhusu waamini wa dini tofauti. Uhuru
wa kuabudu katika ulimwengu wa leo, unaonekana kutetereka kutokana na hali ya watu
kutofahamiana na badala ya kutafuta mambo ambayo yanayojenga, kila mtu anajiona kuwa
bora zaidi kuliko mwingine na mjuaji zaidi, mambo ambayo kimsingi yanasababisha chuki
na uhasama ndani ya Jamii.
Anasema kwamba, katika maisha na utume wake kama
Rabbi sehemu mbali mbali, na baada ya kushinda hali ya kujiona kwamba imani yake ilikuwa
ya maana zaidi kuliko imani za wengine ambazo hata hakuzifahamu kabla, aliweza kushirikiana
na baadhi ya viongozi wa dini mbalimbali kwa ajili ya kusaidia kuanza mchakato wa
majadiliano ya kidini, ili kuweza kuleta maelewano katika jumuiya mbalimbali za waamini.
Anasema kuwa, ikiwa kila mtu atajitahidi kuuona uwepo wa Mwenyezi Mungu ndani
ya kila mwanadamu, hapo kwa hakika, ataweza kumheshimu na kumpenda na kuingia katika
ushirikiano na yeye, hali ambayo haiwezi kuacha kuleta mabadiliko katika jamii; kwani
jukumu la kila mmoja wao ni kuhakikisha kwamba haki, usawa na amani vinakuwepo katika
ulimwengu mamboleo.
Rabbi Mkuu David Rosen anaendelea kusisitiza kwamba kama
mtu anathamini amana za kibinadamu kama vile utu, ili aoneshe uaminifu katika kile
anachokiamini anatakiwa kuwa tayari kuingia katika majadiliano ya kina na watu wengine
bila kujali tofauti zao.
Hili linatokana na ukweli kwamba, ikiwa watu wanang’ang’ania
ubinafsi wao na hali ya kutokuelewana, vitendo vya jinai vitaongezeka badala ya kukumbatia
majadiliano ya kidini na kiekumene ambayo yanatija zaidi katika utamaduni wa dini
mbalimbali. Mara nyingi, dini imetumika vibaya kwa ajili ya mafao ya watu binafsi,
na hili linatokana na ukweli kuwa kila mtu anajisikia kuwa na madaraka ya kutumia
dini kwa manufaa yake binafsi, jambo ambalo ni hatari sana.
Padre Edward Daleng
wa Shirika la Waaugustiani kutoka mjini Jos, Nigeria ameelezea ni jinsi gani Shirika
la kitawa la Mtakatifu Augostini linavyojitahidi kusaidia shughuli za majadiliano
ya kidini kati ya waamini wa dini ya kiislam na wale wa dini ya Kikristo. Anaeleza
kwamba kumetokea hali ya kutoaminiana katika jamii ya Wanaigeria baada ya matukio
ya kujitoa mhanga nchini humo kuongezeka kwa kasi.
Ili kuondokana na hali
hiyo ya kutoaminiana, anasema kwamba Shirika la Mapadre wa Agostiniani, kwa kushirikiana
na baadhi ya mashirika yasiyo ya kiserikali yanayofanya kazi nchini humo, yameamua
kulivalia njuga swala hilo ili kulipatia suluhu ya uhakika.
Anasema, kunako
mwaka 2005 Mapadre hao wakishirikiana na mashirika mbali mbali walianzisha programu
ya maendeleo jamii: kwa kuanza na kujenga shule za msingi ambamo wanafunzi wanaotoka
kwenye familia za dini ya Kiislam na wale wa kutoka kwenye dini za Kikristo wanasoma
pamoja na kucheza pamoja. Vile vile wamefanikiwa kujenga shule za sekondari ambamo
pia wanafunzi wa dini hizo mbili wanasoma pamoja kwa amani na utulivu mkubwa; wakijifunza
utamaduni wa kukubali na kupokea tofauti zao kwani hao ndio watakao kuwa viongozi
wa nchi yao kwa kizazi kijacho,
Jambo hili linasaidia kukuza utamaduni mpya,
utamaduni wa majadiliano na amani. Kuna vituo kwa ajili ya kuwawezesha akina mama
kwa kuwapatia kozi mbalimbali zinazowasaidia kujiaajiri ili kukidhi mahitaji yao
na ya familia zao; vituo ambavyo kila mwaka vinapokea idadi ya akina mama wapatao
250.
Hata katika vituo hivi, kina mama wanaofadika na huduma hizo ni wale
wanaotoka kwenye imani mbalimbali zikiwemo za kikristo na kiislam. Wote wanajifunza
mambo kwa pamoja na kushirikishana vipaji vyao bila ubaguzi wowote. Mambo haya yanaleta
utamaduni mpya katika jamii kwani kina mama hawa wanaporudi majumbani mwao wanajaribu
kuelezea mambo mazuri wanayojifunza kutoka katika vituo hivyo, na hili, taratibu linaleta
mwelekeo mpya na utamaduni wa kuthaminiana kila mtu katika utofauti wa imani yake,
kiasi kwamba, wanawake wanakuwa kweli ni vyombo vya amani, upendo na mshikamano katika
Jamii.
Katika kutafuta jinsi ya kuwasaidia vijana ili waweze kuelekeza nguvu
zao katika mambo yanayowajenga na kukuza utamaduni wa kuheshimu tofauti za wengine,
Shirika la Mapadre pamoja na wadau wao wameunda timu ya mpira kwa wavulana, ambayo
inaundwa na vijana wa dini ya Kiislam pamoja na ile ya Kikrsto. Timu hiyo pia imekuwa
ni kichocheo kwa baadhi ya viongozi wa dini ya Kiislam na ile ya Kikrsto kuungana
na kufanya kazi pamoja katika harakati za kutaka kuondoa hisia za kutoaminiana, kupokeana
wala kuheshimiana.
Juhudi zote hizi zinalenga kuleta upatanisho kati ya makundi
mbalimbali kwenye jamii ya wananchi wa Nigeria. Jambo hili, taratibu linaanza kuonesha
mafanikio yake kwani watu wameanza kurudisha imani kati yao. Amehitimisha mada yake
kwa kutumia maneno ya Mtakatifu Augustino, Askofu na Mwalimu wa Kanisa aliyesema kwamba
“Yule ambaye kweli anapenda amani, anawapenda hata maadui wa amani.”