2013-04-20 11:17:15

Utakatifu na ukweli; upendo na mshikamano pamoja na Uinjilishaji mpya ndiyo changamoto iliyopo kwa sasa!


Uchaguzi wa Baba Mtakatifu Francisko ni changamoto kubwa kwa waamini kutoka Amerika ya Kusini kuchuchumilia utakatifu wa maisha; ukweli na umoja; upendo na mshikamano pamoja na Uinjilishaji mpya. Haya ni mambo muhimu sana yanayopaswa kupewa msukumo wa pekee katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo.

Ni changamoto inayotolewa na Kardinali Marc Ouellet, Rais wa Tume ya Kipapa ya Amerika ya Kusini, kama sehemu ya kumbu kumbu ya mwezi mmoja tangu Baba Mtakatifu Francisko alipochaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki. Huyu ni Papa wa kwanza kutoka Shirika la Wayesuit na Papa wa kwanza kutoka katika nchi za Amerika ya Kusini.

Hili ni tukio la pekee kabisa katika historia ya Kanisa Katoliki. Kutokana na ukweli huu, waamini na wananchi kutoka Amerika ya Kusini wanapaswa kujisikia kuwa karibu zaidi na Khalifa wa Mtakatifu Petro, ili Amerika ya Kusini iweze kuwa ni chemchemi ya matumaini mapya. Wajiunge na kutengeneza mnyororo wa sala kwa ajili ya kumwombea Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume wake kwani kwa hakika anahitaji sala na sadaka yao.

Uwe ni mwendelezo wa maombi yanayoendelea kutolewa na Baba Mtakatifu Francisko kwa watu mbali mbali ili waweze kumsindikiza katika Sala zao. Baba Mtakatifu aweze kuwa karibu zaidi na waamini aliokabidhiwa kwake na Kristo kama Khalifa wa Mtakatifu Petro, akitoa kipaumbele cha kwanza kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii ili waweze kuonja na kufarijika na huruma na upendo unaobubujika kutoka kwa Kristo Mkombozi wa ulimwengu.

Kardinali Marc Ouellet anawachangamotisha Maaskofu Katoliki kutoka Amerika ya Kusini kujiuliza ndani mwao maana na dhamana ya utume wao Amerika ya Kusini, sehemu ambayo ina nafasi ya pekee katika moyo wa Baba Mtakatifu Francisko. Ni mwaliko na changamoto ya kupiga moyo konde na kusonga mbele kwa matumaini huku wakimtangaza na kumshuhudia Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kutoka katika wafu. Mwishoni, anawaalika Maaskofu kuonesha upendo na mshikamano wa dhati kwa Baba Mtakatifu Francisko.







All the contents on this site are copyrighted ©.